JUA NAMNA TANO (5) YA KUUZA KWA KUTEKA HISIA ZA MTEJA


Hivi umewahi nunua kitu wakati ukiwa na furaha sana halafu baadae ukajikuta unajutia maamuzi ya manunuzi yako?


Au yale maamuzi ya kitu fulani ulinunua kwasababu ya uwoga tu uliokua nao kwa kuogopa labda kile kitu kitaisha,ukajikuta unanunua haraka haraka.


Halafu siku zinaenda unakuta kile ulichonunua hakina manufaa au kinaendelea kuwepo lakini wewe uliogopa ukajua baadae huenda kitaisha dukani n.k

Hizo ni baadhi ya hisia ambazo huwa zinawakuta watu na hujikuta wakifanya maamuzi kwa kuendeshwa na hisia badala ya fikra za kimantiki(logic). 


Kuuza kwa kuzingatia hisia alizonazo mteja ni jambo la msingi kuliko hata huduma au bidhaa yako ilivyo.


Kwani huwa inaaminika kuwa watu huwa wananunua vitu/huduma kutokana na hisia watakazopata kutoka kwenye hiyo huduma/bidhaa kuliko hata,namna bidhaa au huduma hiyo ilivyo. 


Hii kwa maana nyingine ni kuwa watu huwa wananunua kutokana na namna watakavyojisikia wakiwa na kitu ulichowauzia.


Hisia anazokuwa nazo mteja zinaweza kuwa kama hisia za furaha atakayopata,hudhuni itakayoondolewa na bidhaa yako,uwoga alio nao,au hasira za mteja. 


Sasa unapouza bidhaa au huduma yako hakikisha unamteka mteja kulingana na hisia alizo nazo kwa wakati huo.

Kuna baadhi ya mbinu za kuuza kulingana na hisia za unazoweza kuzitumia ili kumdaka mnunuaji kama ifuatavyo:


  • 1.ELEZEA HATARI YA YEYE KUTONUNUA(KUMTISHA)

Njia hii huwa inamfanya mtu achukue maamuzi haraka haraka ya kununua kitu. Kwani unakua umempa hisia za kumtisha kuwa kitu hiki muda si mrefu hutakipata tena. 

Au unamuonyesha hatari/hasara atayopata kama hatachukua maamuzi ya kununua kile unachouza.


Mfano: Upo kwenye kampuni ya kuuza BIMA unaweza kumtisha mteja na kumuelezea hatari atakazokutana nazo kwa kuendesha chombo cha moto bila kuwa na bima,kama “ukikamatwa na askari wa usalama barabarani kwa kuendesha gari hili bila bima atakupiga faini au utapelekwa mahakamani”



Hapo unakua umeamsha na kukumbusha hisia mteja madhara atakayopata kwa kuendesha gari bila bima na hivyo atafanya maamuzi haraka ya kununua BIMA unayouza. 

Je kwa bidhaa au huduma unayouza unajua hasara au madhara atayopata mtu kama akiikosa? Jiulize hilo


  • 2. ELEZEA NAMNA ITAKAVYOMPA THAMANI

Hivi unadhani ni kwanini watu wanaomiliki bidhaa zenye gharama na brand kubwa huwa wanalinga?


Bidhaa zenye majina makubwa na za gharama kama magari ya thamani,simu kama Iphone,saa za thamani huwa zinamfanya mtu ajione yeye ni wa kipekee sana.



Sasa na wewe wakati unaelezea bidhaa au huduma yako elezea namna itampa thamani na kuonekana watofauti na wengine. 

Watu huwa wanapenda vitu vizuri na vya kipekee ambavyo wengine hawana.


Watu huwa wanapenda wasifiwe na waonewe wivu,hivyo zingatia kuteka hisia za mteja kwa kumuaminisha kuwa hii unayo muuzia mtu mwingine hawezi kuwa nayo kiurahisi.

  • 3.ELEZEA HISIA ZA KUPATA MATOKEO YA KARAKA

Hii huwa ni mbinu ya kuuza kwa kuteka hisia za mtu kwa kumuaminisha kuwa atapata matokeo ya haraka. 


Au kuonyesha ni kwa namna gani bidhaa au huduma yako itatatua tatizo lake kwa haraka na atapata matokeo mazuri. 


Mfano: Unadhani ni kwanini wauza madawa ya kupunguza uzito huwa wanasema “Ukitumia hii utapunguza zaidi ya kilo 5 ndani ya wiki 2?


Hapo unakua unateka hisia za mteja na kumuaminisha kuwa hii bidhaa inafanya kazi haraka haraka unapata matokeo maana unajua kabisa kuwa watu huwa wanapenda matokeo ya haraka au makubwa kwa gaharama ndogo. 


Sasa teka hisia za mteja wako kwa kutumia njia hii kulingana na aina ya mteja na mazingira.


  • 4. ONYESHA AIBU ATAKAYOPATA

Hivi umewahi kutana na muuzaji anakwambia “wewe nae hadi leo unatumia simu ya tochi huoni aibu,tazama hii smartphone ilivyo nzuri takuuzia kwa bei ya punguzo”


 Au mwingine anasema “acha kutumia magauni ya zamani njoo kwetu upate mikato mipya”.

Hapo ni muuzaji anakua yupo kwenye kuteka hisia za mteja kuwa usiponunua hiki cha kwangu utakua nje ya fasheni na utaachwa nyuma na wakati na utakua unatia aibu. 


Hulka ya binadamu huwa hawapendi aibu ndio maana huna maamuzi ya kununua huwa yanafanyika ili kukwepa aibu.


  • 5. ONYESHA HISIA ZA KUMFIKISHA MALENGO YAKE

Hii ni mbinu ya kumuonyesha mteja wako ni namna gani atafikia malengo yake kwa kutumia bidhaa au huduma uliyo nayo. 


Mfano “Ukitumia mbolea hii nayo kuuzia wakati wa kupanda mazao yako utavuna zaidi ya magunia 100 kwa hili shamba lako tofauti na sasa unapata magunia 40 tu”

Au “Ukinunua kiatu hiki ni cha Ngozi utakaa nacho miaka mitatu bila kununua kiatu kingine kwasababu ni kigumu na kina dumu muda mrefu”. 


Hapa unakua umeteka hisia za mteja anaona faida atayopata na atakua ametimiza malengo yake kwa kufanya maamuzi ya kununa bidhaa au huduma yako.

Je,wewe unajua namna ya kuielezea bidhaa au huduma yako ili mteja aone faida atakayopata toka kwako?  



KUMBUKA: Kuuza kwa mafanikio unahitaji ufahamu vizuri mtu unaemuuzia,mahitaji na maumivu anayopitia,kitu gani anapenda,ana hamasika na nini,na hisia zake zinatekeka kiurahisi na nini. 


Pia unatakiwa uwe na lugha ya ushawishi,na vile vile onyesha feedback nzuri za wateja uliowauzia bidhaa au huduma yako ili kuongeza ushawishi zaidi.



IMEANDIKWA NA

Mchumi Consulting

0714260266

BONYEZA HAPA KUONA HUDUMA ZETU NYINGINE


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FAIDA ZA KUWA NA KAMPUNI NA NAMNA YA KUGAWA HISA NA KUISAJILI HAPA TANZANIA