FAIDA ZA KUWA NA KAMPUNI NA NAMNA YA KUGAWA HISA NA KUISAJILI HAPA TANZANIA
Kampuni ni chombo muhimu katika ulimwengu wa biashara, kinachowezesha watu kuunganisha rasilimali zao na kufanya shughuli za kiuchumi kwa pamoja.
Kampuni inaweza kuwa na umiliki wa watu binafsi, familia, au hata wawekezaji wengi. Katika muktadha wa Tanzania, kampuni ni njia bora ya kuendesha biashara kwa ufanisi na kupata faida kubwa.
MAANA YA KAMPUNI
Kampuni ni asasi au shirika linalotambulika kisheria ambalo limeundwa kwa ajili ya kuunda au kuuza bidhaa na/au huduma kwa wateja.
Kampuni ina sifa ya kuwa na utu wa kisheria tofauti na wamiliki wake, kumiliki mali zake, na kuwa na uwezo wa kushtaki na kushtakiwa kwa jina lake.
Faida za Kuwa na Kampuni
1.Utu wa Kisheria:
Kampuni inatambulika kisheria kama mtu binafsi, tofauti na wamiliki wake. Hii inamaanisha kuwa kampuni inaweza kumiliki mali, kuwa na madeni, na kuingia mikataba kwa jina lake.
2.Uwezo wa Kukusanya Mtaji:
Kampuni inaweza kukusanya mtaji kwa kuuza hisa kwa wawekezaji. Hii inasaidia kampuni kupata fedha za kuendesha na kukuza biashara.
3.Uwezo wa Kudumu:
Kampuni ina uwezo wa kudumu hata kama wamiliki wake watafariki au kujiondoa. Hii inahakikisha kuwa biashara inaendelea bila kuathiriwa na mabadiliko ya wamiliki.
4.Uwezo wa Kupata Mikopo:
Kampuni inaweza kupata mikopo kwa urahisi kutoka kwa taasisi za fedha kama benki, kwa sababu ina utu wa kisheria na inaweza kutoa dhamana.
5.Uwezo wa Kupanua Biashara:
Kampuni inaweza kupanua biashara zake kwa urahisi kwa sababu ina uwezo wa kuvutia wawekezaji na kupata mikopo kwa urahisi.
SOMA PIA MAMBO YA KUZINGATIA NA KUTOFANYA WAKATI WA KUANZISHA KAMPUNI
HISA ZA KAMPUNI NI NINI?
Hisa za kampuni ni sehemu ya umiliki wa kampuni. Hisa moja inawakilisha asilimia ndogo ya umiliki katika kampuni hiyo.
Kwa mfano, kama kampuni ina hisa milioni moja na mwekezaji anamiliki hisa 10,000, basi mwekezaji huyo anamiliki 1% ya kampuni.
Wanahisa (wamiliki wa hisa) wana haki ya kushiriki katika maamuzi ya kampuni kupitia mikutano ya wanahisa na pia wanapata gawio (faida) kulingana na idadi ya hisa wanazomiliki.
Hisa zinaweza kununuliwa na kuuzwa kwenye soko la hisa, na thamani yake inaweza kupanda au kushuka kulingana na utendaji wa kampuni na hali ya soko.
NAMNA YA KUGAWA HISA ZA NDANI YA KAMPUNI
Hivi ndivyo unaweza kugawa hisa ndani ya kumpuni husika
1.Kuamua Jumla ya Hisa:
Kwanza, amua jumla ya hisa ambazo kampuni yako itakuwa nazo. Hii inaweza kuwa, kwa mfano, hisa 1,000,000.
2.Kuamua Mgawanyo wa Hisa:
Amua jinsi hisa hizo zitakavyogawanywa kati ya wamiliki wa kampuni.
Hii inaweza kufanywa kwa kuzingatia mchango wa kila mmiliki katika kampuni, kama vile mtaji waliowekeza au kazi wanazofanya.
3.Kuweka Kumbukumbu za Hisa:
Andaa rejista ya wanahisa ambayo inaonyesha jina la kila mmiliki na idadi ya hisa wanazomiliki. Unaweza kutumia programu za usimamizi wa hisa au hata Excel kwa kuanza.
4.Kusajili Mabadiliko:
Ikiwa kuna mabadiliko yoyote katika umiliki wa hisa, kama vile kuuza au kuhamisha hisa, ni muhimu kusajili mabadiliko hayo katika rejista ya wanahisa na kuhakikisha kuwa nyaraka zote za kisheria zinasasishwa.
5.Kutoa Vyeti vya Hisa:
Kila mmiliki wa hisa anapaswa kupewa cheti cha hisa kinachoonyesha idadi ya hisa wanazomiliki. Cheti hiki ni uthibitisho wa umiliki wa hisa na kinaweza kutumika kama nyaraka rasmi.
JINSI YA KUISAJILI KAMPUNI TANZANIA
1.Kusanya Taarifa za Wahusika:
Wahusika ni wanahisa, wakurugenzi, na katibu wa kampuni. Hakikisha una taarifa zao zote muhimu.
2.Andaa Nyaraka za Usajili:
Nyaraka hizo ni Memorandum of Association, Articles of Association (Memarts), na Declaration of Compliance (Form 14b).
Memarts lazima isainiwe na waasisi wa kampuni na kuwa na muhuri wa mwanasheria.
3.Jaza Maombi kwenye BRELA ORS:
Jaza taarifa zote ulizokusanya kwenye mfumo wa BRELA ORS (ors.brela.go.tz).
4.Download Nyaraka toka BRELA ORS:
Baada ya kujaza maombi, download consolidated form na integrity form, kisha msaini na kuweka tarehe.
5.Upload Nyaraka kwenye BRELA ORS:
Scan nyaraka zote na upload kwenye BRELA ORS.
6.Lipia Maombi BRELA:
Utapewa bili yenye control number ambayo utapaswa kuilipia. Ukishalipia, maombi yataenda BRELA kwa dhumuni la kufanyiwa kazi.
7.Subiri Maombi Yafanyiwe Kazi:
Maombi yatafanyiwa kazi na utapokea ujumbe kwa njia ya email ukikueleza kuwa maombi yamepitishwa na cheti kipo tayari kupakuliwa.
MWISHO
Kusajili kampuni na kugawa hisa ni hatua muhimu katika kuanzisha na kuendesha biashara kwa mafanikio.
Kampuni inatoa faida nyingi kama vile uwezo wa kukusanya mtaji, kudumu kwa muda mrefu, na kupata mikopo kwa urahisi.
Ni muhimu kufuata taratibu za kisheria na kuwa na mpango mzuri wa usimamizi wa hisa ili kuhakikisha mafanikio ya kampuni yako.
Mchumi Consulting
0714260266
Maoni
Chapisha Maoni