FAHAMU MAKOSA 8 WANAYOFANYA WAUZAJI WAKATI WA KUUZA BIDHAA/HUDUMA ZAO
Kufanya mauzo ni sanaa tunasema “sale is art”,maana yake ni inahitaji kipaji na ujuzi ili kuwa muuzaji mzuri.
Kama ilivyo kwenye mchezo wowote,ili kupata mafanikio ni muhimu,kufanya mazoezi,kufanya makosa,na kujifunza zaidi na pia kutokata tamaa pale unaposhindwa kupata matokeo uliyokuwa unayategemea.
Hapa tutazungumzia makosa kadhaa ambayo wauzaji(sales person) wengi huyafanya pale wanapotaka kuuza bidhaa au huduma waliyo nayo kwa mteja mpya.
Yawezekana unafahamu baadhi ya step muhimu wakati wa kuuza bidhaa au huduma yako kwa mara ya kwanza hasa kwa mteja mpya,asie kufahamu na huenda haifahamu bidhaa yako pia.
Kuna aina fulani ya makosa ambayo wengi wamekua wakiyafanya wakati wa kushawishi kuuza huenda ni bidhaa au huduma fulani.
1. KUONGEA SANA NA KUTOSIKILIZA
Ni muhimu kuongea wakati wa kufanya mauzo na kushawishi mauzo ya bidhaa au huduma yako,lakini kuongea sana wewe peke yako kama muuzaji huwa haina tija sana na mwisho utaishia kumchosha mteja mtarajiwa.
Badala yake tumia muda mwingi katika kusikiliza na kuuliza maswali ili uweze kujua hitaji la mteja hasa ni lipi.
Tafiti zinaonyesha wataalamu wengi wa mauzo huwa hawaongei zaidi ya 40% na badala yake huwaacha wateja watarajiwa waongee na kusikiliza kwa 60% iliyobakia.
Ni muhimu kuzingatia kuuliza maswali na kumsikiliza zaidi mteja,usifikirie kwenye kupata fedha tu na kumuwinda mteja hapana utashindwa kupata wateja.
Tunasema ongea kwa asilimia 40 na sikiliza kwa asilimia 60 zilizobakia.
Kusikiliza zaidi na kumuuliza maswali mengi mteja inafanya akurahisishie kazi yako,maana utajua maumivu yake ni yapi anayopitia na hitaji lake la msingi ni lipi.
2. KUTOA USHAURI BILA KULIPWA
Sio vibaya sana kutoa ushauri kwa mteja mtarajiwa lakini kutoa ushauri zaidi bila uhakika kwa kulipwa chochote au mteja kununua huwa haileti tija sana.
Miongoni mwa madhara yanayopatikana baada ya kuongea sana badala ya kusikiliza utajikuta utaongea na kutoa hadi ushauri bila kupata malipo yoyote na mteja asinunue kitu unachouza.
Kumbuka kuwa na taarifa ni mtaji kwako(information is power),sasa kama utaishia kuwa mzungumzaji zaidi ya kuwa msikilizaji utajikuta unaishia kupewa asante na wateja hawatanunua unachouza.
Usipende kutoa ushauri bila kulipwa chochote.
Badala yake toa suluhisho la bidhaa au huduma yako kwenye process ya kuuza hiyo bidhaa au huduma husika.
Acha kuongea zaidi hata taarifa ambazo hazihusiani na bidhaa au huduma yako na ambazo hazitaleta manufaa kwenye kumdaka mteja husika
3. KUTOJIKITA KUTOA SULUHISHO
Muuzaji hutakiwi kuelezea muonekano au teknolojia ya huduma au bidhaa unayouza badala yake zingatia kwenye kuelezea ni namna gani huduma au bidhaa yako itampa suluhisho mteja husika.
Yale mambo ya kuelezea muonekano au bidhaa hii ina hiki na hiki haita kusaidia sana kwenye kufunga mauzo yako.
Badala yake jikite kwenye kueleza ni kwa namna gani bidhaa au huduma itaondoa maumivu ya mteja au ni namna gani bidhaa au huduma yako itasaidia kumfikisha mteja kutimiza malengo yake.
Kumbuka ni muhimu kuelewa kuwa mteja wako mtarajiwa hahitaji kujua ni namna gani unafanya au kutoa huduma yako au ni namna gani bidhaa yako inafanya kazi ILA anachotaka ni bidhaa au huduma yako itamsaidieje.
Kumbuka ule msemo wa kuwa muonekano wa bidhaa huwa unaishia tu kusema lakini faida zitokanazo na bidhaa huwa ndio zinazouza(“features tell,benefits sell”)
4. KUJIKITA KWENYE BEI NDOGO BADALA YA THAMANI
Watu huwa wananunua thamani sio bei husika.
Kama bado unaamini kuwa bei ndogo ndio itakufanya uuze badala ya thamani ya bidhaa au huduma yako jua bado upo umelala na unaendelea kuota ndoto.
Unaambiwa zaidi ya asilimia 70% ya wanunuaji(wateja) wengi huwa wanasema ni muhimu kuwa na mahusiano ya kudumu na muuzaji au mshauri ambae ni muaminifu na anaeongeza thamani ya bidhaa au huduma anayouza.
Kutegemea kupunguza bei ya bidhaa,kuwa na promotion za mara kwa mara kwa nia ya kuwadaka wateja huwa inafaida kwa mwanzoni lakini sio kwa malengo ya muda mrefu(long term goals)
Hawa wateja wanaokuja kwasababu unawapa punguzo la bei,watakuja kwako leo kwasababu una bei za chini lakini akitokea muuzaji mwingine mwenye bei za chini zaidi yako watenda kwa huyo muuzaji na watakukimbia wewe.
Ingawa bei ndogo huangaliwa kama kivutio kikubwa kushawishi wateja lakini thamani ya bidhaa au huduma inayotolewa ikiwa kubwa hufanya watu wanunue hata kama bei ni kubwa,hivyo zingatia kuongeza thamani bidhaa au huduma yako.
5. KUTOA AHADI NYINGI ZA UWONGO
Kutoa ahadi nyingi za bidhaa au huduma yako na kutotimiza ahadi husika ni sawa na kuidanganya biashara yako.
Haijalishi ni kiasi gani unahitaji kuuza kutoa ahadi nyingi tena za uwongo ni njia mbaya katika kufikia mahusiano ya kibiashara.
Kuficha madhaifu ya huduma au bidhaa yako na kuelezea vitu ambavyo huna haitakufikisha popote.
Cha kufanya ni kuhakikisha unaongea vitu vya kweli kuhusu bidhaa au huduma yako na usitoe ahadi nyingi na kumpa mteja matarajio makubwa sana kuhusiana na bidhaa au huduma husika.
Tunasema toa ahadi kidogo ila mpe matokeo makubwa ambayo alikua hayategemei,itafanya kujenga uaminifu na mteja atakusaidia kukusema vizuri hata kwa watu wengine (underpromise and over deliver).
Bora kutouza kabisa kuliko kutaka kutengenenza mauzo kwa ahadi za uwongo. Maana mteja akigundua kuwa umetoa ahadi ya uwongo ambayo bidhaa au huduma yako haina jua utampoteza na utakosa kuuza siku nyingine na atakupa reference mbaya hata kwa watu wengine na heshima ya brand yako itashuka.
6. KUTOKUA TAYARI KUPATA MAPINGAMIZI(Objections)
Wauzaji wengi huwa hawapendi kukutana na majibu ya “hapana”,na ndivyo ilivyo hata katika maisha ya kawaida jibu la “hii haifai” au “sitaki” huwa linaumiza sana.
Sasa fahamu siri hii kuwa unapokutana na majibu ya “hapana” mara kwa mara kwa mteja jua ndio unatengenenza thamani ya jibu la “ndio”mbele ya safari.
Ndio maana kuna baadhi ya wauzaji huwa wanatumia mbinu hii kwa kukuonyesha bidhaa za kawaida kwanza huku bidhaa nzuri ikiwa ya mwisho kukuonyesha.
Wauzaji hawa kwao neno “hapana” huwa haliwasumbui maana anajua akikuonyesha bidhaa au ofa kadhaa za kawaida au ambazo sio nzuri ukizikataa anajua ile bidhaa au Ofa nzuri atakuonyesha mwishoni na anajua kisaikolojia lazima utakubali na kusema “sawa” “bora hii” maana utakua umechoka kuona bidhaa au ofa usiyoitaka.
Kupambana na mapingamizi ya kununua toka kwa mteja ni sanaa pia,kwani ni muhimu kuwa mtulivu,kuonyesha kuwa unasikiliza lalamiko au hitaji la mteja,na ni muhimu kumjibu kwa utulivu na heshima.
Ukikutana na pingamizi la kukasirisha au kukudhihaki nawe usipaniki,badala yake kuwa mtulivu na jibu kwa heshima na usianze kujibishana na mteja.
Mwisho kama kumjibu na kumuelekeza vizuri bado hakujaleta dalili za matumaini ya kuuza basi jua huyo sio ridhiki yako.
Uwezo wa kugundua kwa haraka wateja ambao sio wanunuaji na ambao ni wapoteza muda ni ujuzi muhimu unaotakiwa kuufahamu wewe kama muuzaji.
Na tafiti zinaonyesha kuwa angalau asilimia 50% ya watu huwa sio wateja kwa ajili ya huduma au bidhaa yako hivyo usipaniki.
7. KUBISHANA NA MTEJA MTARAJIWA
Jambo hili linaweza kuonekana kama jambo la kawaida maana wauzaji wengi wa bidhaa au huduma hufikia wakati huanza kubishana na mteja mtarajiwa,kwa sababu tu amepewa pingamizi asilolipenda toka kwa mteja mtarajiwa(potential customer) acha hii tabia nasisitiza acha kabisa.
Jua kubishana na mteja mara zote hupelekea kupoteza uzo na wauzaji wengi wanaobishana na wateja mara nyingi hushindwa kuuza bidhaa au huduma husika kwa mteja.
Kama hukubaliani na pingamizi la mteja au kitu anachokisema basi mjibu kwa upole ,sema maneno kama “nakusikiliza na nakuelewa sana boss” au “nimeelewa unachomaanisha” na pia muulize maswali ili kumuelewa zaidi na kuelewa anacho kimanisha lakini USIBISHE.
Lakini kama unaendelea kukutana na kizingiti zaidi ni busara na sio mbaya ukaachana na mtu huyo na ukaelekeza focus yako kwa watu wengine/fursa nyingine,maana mwisho wa siku SIO kila mtu atakua mteja wako.
8. KUTOONYESHA UHARAKA
Moja ya mambo ya msingi ambayo yanachukuliwa kawaida na wauzaji wengi ni hili la kuonyesha uharaka wa maamuzi ya mteja kununua.
Hapa ni kuonyesha kuwa mteja anatakiwa afanye maamuzi sasa na sio siku nyingine,kwa maana kwamba hatakiwi kuahirisha.
Muuzaji unatakiwa uonyeshe mazingira ya uharaka na kuhitajika kwa haraka kwa huduma au bidhaa husika.
Unaweza kutumia mbinu mbalimbali kama kuweka deadline (tarehe ya mwisho) au Ofa ya muda maalumu.
Vilevile unaweza weka vivutio mbalimbali kama punguzo la bei ya bidhaa yako na hivyo mteja anatakiwa afanye maamuzi ya busara ya kununua sasa bidhaa au huduma.
Na pia unaweza ukaonyesha shuhuda au feedback nzuri za wateja waliotumia bidhaa au huduma yako ili kumpa hamasa mnunuaji aone hii bidhaa inatumika na inahitajika sana na watu wengi.
Haya ni baadhi ya makosa yanayofanywa na wauzaji wengi na hivyo kupelekea kukosa mauzo mengi na mwisho wa siku wanaendelea kubakia na bidhaa zao au huduma zao kukosa watumiaji.
Kwa kuelewa makosa haya na mengine unayoweza kuwa unayafahamu itakusaidia kuyaepuka ili kuingiza mauzo au mapato.
Je unayajua makosa mengine ambayo yamekua yakifanywa na wauzaji wengi?,basi usisite kutoa maoni yako kwa kupitia comment hapo chini.
Lakini unaweza wasiliana nasi Mchumi Consulting kwa namba zetu za 0769 218125 au 0714260266.
IMEANDIKWA NA
Paul Mchumi
0714260266
Maoni
Chapisha Maoni