UMUHIMU WA KUWA NA KUMBUKUMBU ZA BIASHARA YAKO



Biashara nyingi huporomoka au nyingine hufa kabisa kutokana na kutokuwepo kwa mikakati bora ya ufuatiliaji mwenendo wa biashara husika. 

Watu wengi hujikuta wamefanya matumizi makubwa mpaka wanajikuta wametumia na mtaji wa biashara.

Hii husababishwa na uzembe wa kutotunza kumbukumbu au taarifa za mapato yanayoingia na matumizi. Biashara yoyote ili iweze kufanikiwa,utunzaji wa kumbukumbu ni nguzo muhimu sana. Kuna msemo huwa unasema “mali bila daftari huisha bila habari”

NI KWANINI WATU HAWATUNZI KUMBUKUMBU ZA BIASHARA?

Kuna sababu kadhaa ambazo huwa zinafanya watu waone shida kutunza kumbukumbu za biashara,tutaziangalia baadhi yake hapa chini.

KUKOSA ELIMU YA KIBIASHARA

Watu wengi huanzisha biashara kabla au pasipo kupata elimu ya kutosha kuhusu mambo muhimu ya kuzingatia katika ufanyaji biashara. Na mojawapo ya elimu hizi ni pamoja na elimu ya utunzaji wa kumbukumbu za biashara. 

Hivyo hujikuta wakipoteza biashara zao pasipo kujua chanzo ni nini.

KUTOITHAMINI BIASHARA

Watu wengine huanzisha biashara pasipo kuwa na malengo au ndoto za kimaendeleo katika biashara hiyo. Wengi huanzisha kwa lengo la kupata tu fedha za kujikimu. 

Watu wa namna hii hujikuta katika hali ya kutoithamini biashara, kwani wakipata kidogo hukitumia na hata pasipo kutunza kumbukumbu zozote na hivyo kujikuta kila siku wakianzisha biashara mpya, kwani ya mwanzo ishakufa.

KUTOKUJUA NJIA RAHISI YA UTUNZAJI KUMBUKUMBU.

Kwa kawaida sisi wanadamu huwa hatupendi kujichosha. Huwa tunapenda kutafuta njia rahisi za kutumika katika kufanikisha maswala yetu, na endapo zikikosekana huwa tunaliona swala hilo kama mzigo mzito. Vivyo hivyo hata katika biashara, ikikosekana njia mbadala katika kutatua jambo, mtu huamua kupotezea pasipo kujua athari zake.

ZIPI NI FAIDA ZA KUWA NA KUMBUKUMBU ZA BIASHARA YAKO

Sasa tuangalie ni kwa namna gani biashara yako itafaidika kama endapo unao utamaduni mzuri wa kutunza kumbukumbu za biashara yako kama ifuatavyo.

1.UDHIBITI WA FEDHA TASLIMU

 kumbukumbu husaidia kudhibiti fedha taslimu, huonyesha kiasi cha fedha ambacho biashara inapaswa  kuwa nacho wakati wowote ule na zinasaidia kuhakikisha kwamba fedha hazipotei.

Mjasiriamali anapaswa kuhakikisha kuwa, kila anapofunga biashara yake anafanya uhakiki wa biashara yake na hasa kufahamu kile ambacho kimepatikana kwa mauzo ya fedha tasilimu.


2. KUFAHAMU NAMNA BIASHARA INAVYOENDELEA

   kumbukumbu zinasaidia kufahamu jinsi biashara inavyoendelea.

   Kwa jinsi kumbukumbu zinavyotunzwa vizuri zinaashiria kwamba, biashara husika inasimamiwa ipasavyo na iko ndani ya udhibiti.

   3. KUJUA FAIDA HALISI YA BIASHARA

 Daftari la kumbukumbu au mfumo wa kutunza kumbukumbu humsaidia mmiliki au mjasiria mali kujua faida halisi ya biashara yake, kwa mfano ili kujua faida halisi ya biashara, ni muhimu kuwa na kumbukumbu sahihi. 

Faida ya biashara inatokana na mapato baada ya kutoa matumizi, hivyo ni dhahiri kuwa ili kupata faida halisi yafaa mjasiriamali kuweka taarifa zake za mapato na matumizi halisi. FAIDA={Mapato –Matumizi(Gharama)}


4. UKUSANYAJI NA ULIPAJI WA MADENI

     kumbukumbu hurahisisha ukusanyaji au ulipaji wa madeni. Kwa mfano kama umechukua mkopo toka taasisi fulani ya fedha, utunzaji wa kumbukumbu utakusaidia kuwa na mpango mzuri wa ulipaji wa mkopo huo. 

Lakini kama hauna ni rahisi sana kulipa riba kubwa ambayo haiendani na pato lako na mwisho wako utafiriska.


  5. KUWEKA UHUSIANO MZURI NA WASHIRIKA WA BIASHARA YAKO

   Utunzaji wa kumbukumbu huimarisha uhusiano na washirika wa biashara. Kwa mfano mtu anapenda kuinua biashara yako au kuwekeza katika biashara yako, kumbukumbu zitatoa dokezo la thamani ya biashara yako. 

Kama hutakuwa na kumbukumbu za biashara ni wazi kuwa hautajua thamani ya biashara yako hivyo utamuuzia mtu kwa hasara.

6. HUSAIDIA KUPATA MIKOPO KUTOKA TAASISI ZA KIFEDHA

Watu wengi hutumia njia ya mikopo toka taasisi za fedha kwa ajili ya kuongeza nguvu katika mitaji yao.

Kamwe huwezi kufanya mazungumzo na taasisi hizo kama huna kumbukumbu sahihi za biashara yako, wakati wote wanahitaji taarifa za biashara husika.
Ili uweze kutembea kifua mbele na  kufanya mazungumzo na taasisi hizo kwa lengo la kukopeshwa, ni vema utunze vizuri kumbukumbu za biashara yako.

Ukweli uko  wazi kwamba kumbukumbu nzuri za biashara hurahisisha maongezi na wadau. 

Pia itakusaidia kujua kama riba utakayo ilipa  ni staili yako au la,wengi wanajikuta wanalipa riba kubwa sana kinyume cha uwezo wa biashara yake.

7. MIPANGO YA BAADAE

kumbukumbu zinasaidia kuwa na mipango ya siku za baadae. Hii ni kutokana na kwamba biashara yahitaji kutathiminiwa uwezo na udhaifu wake ili kuandaa mipango mizuri zaidi kwa siku za baadae.

Hili linaweza kufanyika kwa kulinganisha utendaji wa biashara wa siku zilizopita na hivi sasa. 

Kwa kuwa na kumbukumbu utaweza kufanya ulinganisho wa muelekeo mzima wa biashara kwa kipindi kilichopita na sasa.

MWISHO kama tulivyoona kuna umuhimu mkubwa na ulazima wa kuweka kumbukumbu za biashara yako.

Kwani biashara yoyote yenye utaratibu mzuri wa kuweka kumbukumbu,huwa inakua na muendelezo mzuri na huwa inafikia malengo yake kwa haraka zaidi tofauti na ukiwa unaendesha biashara bila kuwa na utaratibu wa kuweka kumbukumbu.

Hivyo suala la kuweka kumbukumbu za biashara sio tu la lazima lakini lina umuhimu mkubwa.

Imeandikwa na

Mchumi Consulting

0714260266

BONYEZA HAPA KUONA HUDUMA ZETU

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FAIDA ZA KUWA NA KAMPUNI NA NAMNA YA KUGAWA HISA NA KUISAJILI HAPA TANZANIA