MAENEO 10 YA KUPUNGUZA MATUMIZI YAKO ILI USEVU PESA NYINGI
Kukata au kupunguza matumizi katika maeneo kadhaa ni mkakati muhimu ambao utakusaidia kuwa na ziada ya pesa kwa ajili ya matumizi mengine muhimu ya kimaendeleo.
Tunaangazia maeneo 10 ambayo ukiyazingatia itakusaidia kuwa na kiasi kikubwa cha pesa kinachobakia
1. PUNGUZA MATUMIZI YA KODI YA NYUMBA NA BILI
-Pango la nyumba
Kama wewe umepanga ni vizuri kuishi nyumba ya gharama nafuu inayoendana na kipato chako ili kupunguza gharama za kulipa kodi kubwa na mwisho wa siku unajikuta pesa yako nyingi inaishia kulipa kodi.
Fanya utafiti wa sehemu ambako unaweza kupata nyumba nzuri lakini kwa gharama ya chini ili upunguze gharama za pango.
-Bili za umeme na maji
Punguza matumizi ya gharama za umeme na maji kwa kuwa na mikakati mbalimbali kama kuzima taa pale ambapo hazitumiki na kutotumia maji hovyo ili kupunguza gharama za umeme na maji.
2. PUNGUZA MATUMIZI YA VYAKULA
Chakula ni hitaji la muhimu ambalo kila binadamu anahitaji,na kila siku lazima ule.
Pesa nyingi huwa inaenda kwenye chakula hivyo ni muhimu kujua namna ya kubajeti na kupunguza matumizi kwenye eneo hili.
-Nunua kwa wingi(Bulk buying)
Nunua vile vitu ambavyo haviozi kwa wingi mara moja ili kuepuka kununua kitu kimoja kimoja mara kwa mara ili upunguze gharama.
-Nunua kwenye masoko ya kawaida
Pendelea kununa vitu vyako kwenye masoko ya kawaida badala ya kwenda kununa kwenye ma-supermarket makubwa ili kupunguza gharama za manunuzi
-Pika chakula nyumbani
Kupika chakula chako nyumbani ni gharama nafuu zaidi kuliko kula chakula cha kununua mtaani au kwenye mahoteli
3. PUNGUZA MATUMIZI YA USAFIRI
Eneo hili ni sehemu nyingine inayotumia pesa zako nyingi,hivyo ni muhimu kufahamu namna ya kujipanga nalo.
-Tumia usafiri wa umma
Pendelea kutumia usafiri wa umma kama daladala badala ya kutumia gari private au taxi. Hii itakusaidia kusevu kiasi kikubwa cha pesa kwenye eneo hili
-Tembea
Kama huna haraka au sehemu unayokwenda ni fupi basi fanya mazoezi ya kutembea badala ya kutumia usafiri wa kulipia kwenda hapo.
4. PUNGUZA MATUMIZI KWENYE BURUDANI NA STAREHE
Eneo hili nalo hutumia kiasi kikubwa cha pesa zako ni muhimu ukaweka mikakati ya kudhibiti.
-Punguza matumizi ya starehe zisizo na ulazima.
-Punguza matumizi kwenye hafla za kulipia ili uburudike.
-Punguza matumizi ya manunuzi ya pombe au vinywaji ambazo ni starehe zako binafsi.
-Kwa wanaume punguza kuhonga kiasi kikubwa cha pesa kwa wanawake.
Na maeneo mengine yote ambayo unajua haya ni matumizi ya starehe tu lakini sio ya lazima sana kuyafanya.
5. PUNGUZA MATUMIZI KWENYE UNUNUZI WA NGUO
Hili ni eneo ambalo unaweza ukalifanyia kazi kwa kupunguza matumizi ya nguo za fasheni kubwa na kununua nguo za mtumba.
Zipo nguo za mtumba nzuri lakini zinauzwa kwa bei ndogo.
Acha kasumba ya kukimbizana na nguo za fasheni za gharama kubwa kama nia yako ni kusevu kiasi kikubwa cha pesa toka kwenye kipato chako
6. PUNGUZA MATUMIZI KWENYE GHARAMA ZA AFYA.
Hili ndio eneo linaloweza kuchukua kiasi kikubwa cha pesa kama endapo hutaliwekea kipaumbele.
-Jiunge na bima za afya
Ukijiunga kwenye mifuko ya bima za afya ni rahisi kupata huduma za matibabu kwa gharama ndogo ambayo unakua ulilipia hapo awali.
-Jikinge na magonjwa
Zipo njia nyingi za kujikinga na magonjwa kama vile kufanya mazoezi au kula chakula bora na njia nyingine nyingi.
Hii itakusaidia kutotumia gharama kubwa za matibabu na utasevu kiasi kikubwa cha pesa.
7. PUNGUZA MATUMIZI KWENYE MIKOPO
Kama endapo unadaiwa mkopo wenye riba basi tambua kuwa ile riba ni gharama za ziada ambazo unatakiwa wewe ndio ulipe.
-Lipa mikopo yenye riba kubwa
Riba kubwa kwenye mkopo ni gharama,na ili upunguze gharama hizi ni kulipa na kuachana kabisa na mikopo yenye riba kubwa.
-Tafuta taasisi zenye riba ndogo.
Kuna wakati huwezi kuepuka mkopo kwa ajili ya biashara au jambo binafsi,sasa ni muhimu ukafanya tafiti ni taasisi ipi inatoa mkopo kwa riba ndogo ili upunguze gharama za kulipa riba kubwa ambazo kimsingi huwa zinamaliza pesa zako.
8. PUNGUZA MATUMIZI YA VIFURUSHI VYA SIMU NA VING’AMUZI
Siku hizi matumizi ya simu yamekua na ulazima mkubwa sana.
Hili ni eneo linalokula pesa zako sana lakini pia kuna yale matumizi ya vifurushi vya ving’amuzi.
Tafuta vifurushi vya bei nafuu vya simu au vingamuzi kwa kuangalia wastani wa matumizi yako ya bando kwa mwezi ni kiasi gani.
Tumia fursa za WIFI za bure kama zipo,itakusaidia kushusha matumizi yako kwenye eneo hili.
9. PUNGUZA MATUMIZI KWENYE ADA ZA SHULE
Elimu ndio uwekezaji wa muhimu sana ambao ni muhimu wewe binafsi kuwa nao au yawezekana unao Watoto au ndugu unao wasomesha.
Jitahidi upunguze gharama za elimu kwa kutafuta kama ni shule nzuri zinazotoa elimu bora lakini kwa gharama rafiki.
Usimpeleke mtoto wako shule ya gharama kubwa ambayo unajua kuwa huwezi kumudu gharama za shule hiyo.
Unaweza kupata shule nyingine inayotoa elimu bora lakini kwa bei nafuu.
Wewe binafsi unaweza kujiunga na kozi mbalimbali ambazo ni za bure(online free course) kama endapo unataka ujiendeleze kwenye eneo flani.
Siku hizi ukiwa na internet ni rahisi kupata maarifa flani bila kuingia gharama kubwa
10. PUNGUZA KUTOA MICHANGO
Ni kweli tunaishi kwenye jamii ya watu ni muhimu ukawa na mahusiano mazuri na watu.
Kutoa michango ya shughuli mbalimbali kwenye jamii imekua ni jambo la kawaida sana katika jamii zetu.
Sasa sio kila mchango lazima utoe.
Angalia na zingatia ile michango ambayo unajua ina maslahi makubwa kwako na ambayo ni muhimu tu.
Mfano sio kila harusi lazima uchangie nyingine zikupite ili uweze kubakia na kiasi cha pesa kwa ajili ya mambo mengine.
Sio kila kikundi cha kuchangishana lazima na wewe uwepo ili kupunguza hiyo michango ya kila wakati.
Haya ni baadhi ya maeneo ambayo unaweza kuyazingatia na ikakusaidia kupunguza matumizi yako kwa kiasi kikubwa na ukajikuta unabakia na kiasi kikubwa cha pesa kwa ajili ya shughuli nyingine za kimaendeleo
IMEANDIKWA NA
Mchumi Consulting
Whatsap-0714260266
JIUNGE BURE NA GROUP LETU LA BIASHARA HAPO CHINI
Bonyeza link chini kuja kwenye group la wasap
👇👇👇
Maoni
Chapisha Maoni