MAMBO 6 YA KUFANYA PINDI UNAPOSHINDWA KULIPA MKOPO WA BENKI
Malengo ya kuchukua mkopo huwa ni kuingiza kwenye lengo la mkopo hasa biashara kwa ile mikopo ya biashara.
Na matarajio ya mkopeshaji na anaekopeshwa huwa ni mkopo huo kurudishwa kwa wakati kama makubaliano ya mkopo yanavyo sema.
Sasa kuna wakati inatokea mfanyabiashara anashindwa kulipa mkopo husika kutokana na sababu mbalimbali zilizo ndani ya uwezo wake au nyingine ni sababu ambazo zipo nje ya uwezo wake na hakuzitarajia kabisa.
Kuna wakati mfanyabiashara anaweza kutwa na majanga mbalimbali yanayofanya biashara ifungwe au isiendelee kuingiza mauzo kama ya awali au mhusika kukutwa na ugonjwa au kufiwa na sababu nyingine nyingi kama ilivyoainishwa hapo awali.
Sasa ikitokea hali hii ni kipi mfanyabiashara anatakiwa kufanya ili angalau aweze kupata ahueni ya kulipa mkopo wa taasisi ya kifedha au namna nyingine ya kupata msaada juu ya hali hii
1. ONGEA NA MKOPESHAJI
Mara nyingi ni vizuri na muhimu ukipata changamoto ya kulipa mkopo ni vema ukatoa taarifa kwa taasisi au benki iliyokupa mkopo mapaema.
Hii husaidia benki au taasisi ya kifedha kuwa na taarifa rasmi na wao inakua rahisi kurekodi taarifa zao kulingana na taratibu za ndani za taasisi ya fedha.
Maana ni jukumu lao la msingi kujua hali ya kiuchumi ya kila mteja aliekopeshwa kama sehemu ya majukumu yao
Ni vizuri kuongea na mkopeshaji juu ya changamoto husika kuliko kukaa na changamoto peke yako,labda tu kwa uwoga au kwa kuogopa.
Weka mahusiano mazuri na wadau wanaokupa mkopo,kama maafisa mikopo wako n.k
Wafanye wawe marafiki zako,hii itasaidia kupewa mawazo ya kipi cha kufanya maana wao wanajua utaratibu wa ndani wa benki au taasisi husika.
2. OMBA MUDA WA KUREJESHA UONGEZWE
Hili ni jambo la msingi sana nalo kuzingatiwa kwa mfanyabiashara pale anapopata changamoto ya urejeshaji wa mkopo.
Omba benki au taasisi ya fedha ikuongezee muda wa kulipa mkopo wako kwa kusogeza mbele(re-structuring au re-scheduling)
Mkopo wako ukifumuliwa upya na kuongezewa muda utapata ahueni kiwango cha marejesho unayorudisha(installments) kila mwezi au katika mfumo wa muda mliokubaliana na taasisi ya fedha au benki
Mfano kama ulikua kwa mwezi unapeleka benki milioni moja sasa unaweza pata ahueni ukawa unapeleka laki sita kila mwezi.
Hii inakupa ahueni na kuipunguzia mzigo biashara ambayo kimsingi imekosa au uwezo wake wa kulipa(capacity) umepungua.
Na unaweza kupata muda wa kujipanga zaidi kwenye biashara yako bila kuathiri jina na sifa yako kwenye taasisi za kifedha.
Ni vizuri maombi haya ukayaweka katika mfumo wa barua rasmi ili nawe uwe na kumbukumbu na uhakikishe barua hiyo imepokelewa rasmi na wahusika(taasisi au benki) kulingana na taratibu zao za upokeaji wa taarifa au maombi ya mteja
3. OMBA MKOPESHAJI ASIMAMISHE GHARAMA ZA ZIADA
Hili pia ni ombi unaloweza kuomba kwa anaekukopesha,maana kila mkopo huwa una masharti kadhaa wa kadha mnaypokubaliana.
Kuna baadhi ya taasisi au benki huweka kiwango fulani cha asilimia kama ongezeko la ucheleweshaji wa mkopo baada ya muda fulani.
Ongezeko hili linaweza kuwa asilimia kadhaa ya rejesho lako la kila mwezi au namna yoyote mliyokubaliana.
Kimsingi haya maongezeko yanayoongezeka kama gharama za mkopo huwa yanaongeza kiasi cha mkopo wote unaotakiwa kulipa.
Hivyo ili kupunguza gharama hizi ni vizuri kuongea na taasisi iliyokukopesha wasimamise gharama hizi ili uzidi kupata ahueni ya kulipa mkopo wao
Jambo hili ni muhimu sana kulifahamu kama wewe ni mfanyabiashara,na unaweza kuandika kabisa barua rasmi ya kuomba jambo hili lifanyike kama sehemu ya jitihada zako za kuhakikisha mkopo wako unalipwa vizuri na utaelezea kabisa changamoto unazo kutana nazo.
Hii itakusaidia sana kama endapo kuna hatua za ziada unahitaji kufanya ili kuweza kujinasua katika jambo la ulipaji wa mkopo husika.
4. OMBA ULIPE KIDOGO KIDOGO
Hii ni njia nyingine ya muhimu kuzingatiwa kwa mfanyabiashara hasa ambae biashara yake imepata matatizo.
Kama tunavyojua hali ya biashara sio kila siku huwa inakua inafanana,maana kuna muda hali inakua mbaya sana hadi unashindwa kupata pesa ya kulipa mkopo wako kwa wakati kabisa
Ni muhimu sasa kuomba rasmi taasisi ya fedha ikuwekee mazingira mepesi ya wewe uwe unalipa pesa ya rejesho lako kidogo kidogo.
Tofauti na ule mfumo wa tarehe fulani ndio lazima rejesho liwe limekwa.
Hakikisha maombi haya yanakua rasmi kabisa tena ikiwezekana andika kabisa barua au email kwa mkopeshaji ili ajue kabisa ili uwe na kumbukumbu ya ombi lako na wao waeke kumbukumbu rasmi.
Hii itasaidia taasisi ya kifedha au benki,kubadilisha utaratibu na namna ya kuuweka mkopo wako kulingana na taratibu zao za ndani.
Usiwe muoga kutafuta suluhu ya namna ya kulipa mkopo wako pale unapopata matatizo
Ukikaa kimya bila kutoa taarifa ndio husababisha matatizo makubwa baadae ikiwa ni pamoja na kuuziwa dhamana za mkopo husika
5. OMBA ULIPE RIBA NDANI YA MUDA FULANI
Jambo lingine unaloweza ongea na mkopeshaji(benki au taasisi ya kifedha yoyote) baada ya kupata changamoto ya ulipaji ni pamoja na kuomba ulipe riba tu ndani ya muda fulani.
Hii itakusaidia kupata ahueni ya urejeshaji katika wakati huu ambao unapitia changamoto ya biashara.
Na itasaidia uendelee kujipanga zaidi ili huko mbeleni urudi katika mfumo wa awali.
Hii huwafaa zaidi wale ambao wamepata changamoto ya dharula kwa sasa lakini wana uhakika kuwa baadae wataweka sawa mambo yao upande wa biashara.
Mfano kwa yule mfanyabiashara ambae labda mzigo umechelewa kufika,au kuna watu anawadai malipo yamechelewa,au kuna wale wafanyabiashara ambao amepata changamoto ya ulipaji ila huko mbeleni atapata pesa ya uhakika kulipa vizuri rejesho.
Changamoto ya njia hii ni kuwa mwanzoni huku unapata ahueni ya kulipa rejesho dogo(riba tu),lakini huko mbeleni utalipa marejesho makubwa maana marejesho mengi huwa yanasogezwa mbele
6. OMBA MSAADA AU UZA BAADHI YA MALI ZAKO
Jambo jingine unaloweza kufanya ukipata changamoto ya kulipa mkopo,ni pamoja na kuomba msaada kwa ndugu jamaa na marafiki ili wakupe msaada.
Hapa ni unawaelezea ndugu au marafiki hatari unayoiona au inayoweza kutokea kama ukishindwa kulipa mkopo wa taasisi ya fedha au benki ikiwemo suala la dhamana yako kuuzwa.
Hii itakusaidia kupata mawazo mbadala au msaada wa kifedha au kisheria kwa watu,maana wao wanaweza kuwa na uzoefu au wakakusaidia kiasi cha fedha ukaenda kulipa.
Lakini vilevile kama endapo una mali au vitu vya kuuza kwa haraka,unaweza fanya hivyo kwa kuuza ili upate fedha ya kulipa mkopo au kuwekeza kwenye biashara ili ipate mzunguko na kuiongezea nguvu ili urudi katika hali ya kawaida.
Tumeona baadhi ya mambo unayoweza kufanya ili angalau ujinasue hasa pale biashara yako inapokosa uwezo wa kulipa mkopo kwa sababu huenda zilizo nje ya matakwa yako.
Haya ni baadhi tu ya mambo ya kufanya lakini kuna njia nyingine nyingi ambazo zinatofautiana kulingana na aina ya mkopo,mazingira,aina ya mkopeshaji na vitu vinginevyo.
Na pia ikumbukwe sio kila njia iliyotajwa hapo juu inaweza kumfaa kila mtu,maana masharti ya kimkataba yanaweza kuwa yameelekeza kipi cha kufanya kukitokea changamoto ya kushindwa kulipa mkopo kwa wakati au kushindwa kulipa kabisa.
IMEANDIKWA NA
Mchumi Consulting
0714260266
JIUNGE NA GROUP LETU LA WASAP BURE ILI UPATE HUDUMA NA MASOMO YETU MUDA WOTE👇
Maoni
Chapisha Maoni