TOFAUTI KATI YA KUWEKA AKIBA NA KUWEKEZA: IPI INAKUFAA ZAIDI SASA?
Lakini unashangaa kitu kimoja; bidhaa ambazo ungezinunua kwa Milioni 1 miaka miwili iliyopita, leo hii unahitaji Milioni 1 na laki mbili kuzinunua!
Hapa ndipo wengi wetu tunapofeli. Tunasema "tunaweka akiba," lakini kumbe tunaruhusu mfumuko wa bei (inflation) utafune thamani ya jasho letu bila sisi kujua.
Mara nyingi tunasikia watu wakisema kwa fahari, "Naweka akiba kwa ajili ya baadaye," au wengine wakisema, "Natafuta sehemu salama ya kuwekeza."
Lakini, je! unajua kuwa mambo haya mawili ni tofauti kabisa kama ilivyo mchana na usiku? Moja inakulinda na njaa ya kesho, lakini nyingine inakupa utajiri wa kudumu.
Kama kweli una nia ya dhati ya kufika mbali kiuchumi na kuacha kuishi kwa kutegemea mshahara au faida ya biashara ya leo pekee, ni lazima uelewe mstari uliochora tofauti kati ya Akiba na Uwekezaji.
Usipojua tofauti hii, unaweza kujikuta una akiba kubwa benki, lakini bado unazidi kuwa maskini kila siku thamani ya fedha inaposhuka.
Leo, nataka tupasue mshipa huu. Nataka ujue ni lini unapaswa kuweka akiba, na ni lini unapaswa kuwa na ujasiri wa kuwekeza.
1. Kuweka Akiba (Saving) Ni Nini?
Kuweka akiba ni kitendo cha kutenga sehemu ya fedha unazopata sasa hivi ili uzitumie baadae. Hapa lengo lako kuu ni usalama na upatikanaji wa haraka wa fedha hizo pindi unapozihitaji.
Kuweka akiba hakuna hatari kubwa (low risk). Shilingi laki moja uliyoweka leo, utaikuta ni laki moja ile ile baada ya mwezi mmoja.
Mifano ya Akiba:
Mfuko wa Dharura: Fedha unazoweka benki kwa ajili ya matatizo ya ghafla kama ugonjwa au gari kuharibika.
Akiba ya Likizo au Sherehe: Unatenga kidogo kidogo ili mwisho wa mwaka uende mapumziko au ulipe ada ya shule ya mtoto.
Kuweka kwenye Kibubu au Akaunti ya Akiba: Fedha ambazo unaweza kuzitoa wakati wowote kupitia ATM au simu.
2. Kuwekeza (Investing) Ni Nini?
Kuwekeza ni kitendo cha kuchukua fedha uliyonayo na kuitupa kwenye "shamba" fulani ili izae matunda. Hapa lengo lako siyo usalama pekee, bali ni kukuza thamani ya fedha hiyo. Unataka laki moja yako iwe laki moja na elfu ishirini baada ya muda fulani.
Kuwekeza kuna hatari (risk) kidogo, lakini faida yake ni kubwa kuliko akiba ya kawaida.
Mifano ya Uwekezaji:
Hisa: Kununua sehemu ya umiliki wa kampuni (mfano NMB au CRDB) ili upate gawio la faida.
Vipande (UTT AMIS): Kuweka fedha ambapo wataalamu wanazisimamia na kuzizalisha.
Hatifungani (Treasury Bonds): Kukopesha serikali fedha zako na wao wanakulipa faida kila baada ya miezi sita.
Biashara au Majengo: Kujenga nyumba ya kupanga au kuanzisha duka la jumla.
Tofauti ya Msingi (Kwa Mifano Hai)
Tuseme wewe na rafiki yako mna shilingi Milioni 1 kila mmoja leo.
Wewe (Mwekaji Akiba): Unaiweka hiyo Milioni 1 kwenye akaunti yako ya kawaida ya benki. Baada ya mwaka mmoja, utaikuta ile ile Milioni 1 (labda imepungua kidogo kwa makato ya benki). Thamani yake imeshuka kwa sababu bei ya bidhaa mtaani imepanda (Mfumuko wa bei).
Rafiki yako (Mwekezaji): Anachukua ile Milioni 1 na kununua Vipande (UTT) au Hatifungani ya Serikali. Baada ya mwaka mmoja, anaweza kukuta imekuwa Milioni 1 na laki moja na nusu (1,150,000). Hapa fedha yake imeongezeka thamani.
Ipi Inakufaa Zaidi Sasa?
Hili ndilo swali la msingi. Jibu langu ni hili: Unavihitaji vyote, lakini kwa mpangilio maalumu.
1. Tumia "Akiba" Ikiwa:
Bado huna mfuko wa dharura (Emergency Fund). Kabla hujaanza kuwekeza, hakikisha una akiba ya kutosha kuendesha maisha yako kwa miezi 2 hadi 6 bila kufanya kazi(kwa mfanyakazi ukiwa na mshahara wa uhakika ni rahisi zaidi,hiyo pesa ya ziada ukaitupa kwenye Uwekezaji)
Unajua utaihitaji hiyo fedha ndani ya muda mfupi (chini ya mwaka mmoja). Mfano: unataka kununua kiwanja mwezi wa kumi. Hapa usiwekeze kwenye biashara hatarishi, weka akiba.
2. Tumia "Uwekezaji" Ikiwa:
Tayari una akiba ya dharura.
Una fedha ambayo unajua hutaitumia kwa mwaka 1, 3, 5, au 10 ijayo. Hapa ndipo utajiri unapotengenezwa.
Unataka kupambana na mfumuko wa bei (bei za bidhaa kupanda kila siku).
Kumbuka
Kuweka akiba kutakulinda na njaa ya leo, lakini kuwekeza kutakupa uhuru wa kifedha wa kesho. Usiwe mtu wa kuweka akiba tu maisha yako yote; anza kujifunza kuwekeza kidogo kidogo. Hata shilingi elfu kumi inaweza kuwa mbegu ya mti mkubwa baadae.
Paul
0714 260266
PATA KITABU CHA MISINGI YA UWEKEZAJI HAPA

Maoni
Chapisha Maoni