UCHUMI WA BIASHARA: MTEGO WA BEI NA FAIDA-KWANINI BIASHARA NDOGO ZINASHINDWA
Au ushawahi kukutana na mfanyabiashara anayeza bidhaa kwa bei ya juu sana, lakini wateja hawaonekani, na hata wakija wanageuka na kuondoka bila kununua?
Kama jibu ni ndiyo, basi karibu kwenye mtego mkubwa wa "Uchumi wa Bei." Wajasiriamali wengi wadogo nchini Tanzania wanashindwa si kwa sababu hawana bidhaa nzuri, bali kwa sababu hawajui uhusiano kati ya bei, idadi ya mauzo (turnover), na nguvu ya jina la biashara (brand).
Leo tutachambua makosa mawili makubwa yanayoweza kuua biashara yako kabla hata haijakua.
Mtego wa Kwanza: Kuuza kwa Bei Ndogo Wakati Huna Mzunguko Mkubwa
Hili ni kosa namba moja la wafanyabiashara wengi wanaoanza. Unafungua duka au kuanza kutoa huduma, kisha unaamua kuweka bei ya chini sana kwa lengo la "kuvuta wateja."
Shida iko wapi?
Ili uweze kuuza kwa bei ndogo sana na bado upate faida, unahitaji kitu kinachoitwa "High Turnover" (Mzunguko Mkubwa wa Mauzo).
Makampuni makubwa kama supermarkets au viwanda vikubwa vinaweza kuuza bidhaa kwa faida ya TSh 100 kwa kila bidhaa, kwa sababu wanauza bidhaa 10,000 kwa siku. Hiyo ni faida ya Milioni 1 kwa siku!
Lakini wewe mjasiriamali mdogo unayeuza bidhaa 5 tu kwa siku, ukichukua faida ya TSh 100, utapata TSh 500 kwa siku. Je, hiyo TSh 500 itakulipia pango la fremu? Italipa umeme? Itakupa chakula? Jibu ni HAPANA.
Mfano: Fikiria unauza maji ya chupa. Ukiamua kuuza chupa moja kwa faida ya Sh 50 wakati unauza chupa 10 tu kwa siku, utapata Sh 500. Lakini yule anayeuza chupa 1,000 kwa siku, akipata faida ya Sh 50, ana Sh 50,000.
Somo: Kama mauzo yako ni kidogo (low turnover), unahitaji faida kubwa kwa kila bidhaa ili biashara ijiendeshe.
Mtego wa Pili: Kuuza kwa Bei Kubwa Wakati Huna "Brand"
Huku ni upande mwingine wa sarafu. Kuna wafanyabiashara wanataka kupata faida kubwa haraka, hivyo wanaweka bei ya juu (Premium Price). Lakini wanasahau kitu kimoja: Wateja hawalipii bidhaa tu, wanalipia "Imani" na "Hadhi" (Brand).
Wateja wako tayari kulipa TSh 50,000 kwa t-shirt yenye nembo ya brand kubwa inayojulikana duniani, lakini hawako tayari kulipa kiasi hicho kwa t-shirt hiyo hiyo kama haina jina au inatoka kwa mtu wasiyemjua.
Kwanini mauzo yanashuka hapa?
Ukosefu wa Imani: Mteja anawaza, "Nikitoa laki moja hapa, nikigundua bidhaa ni mbaya nitampata wapi huyu mtu?"
Ulinganifu wa Soko: Mteja atakuuliza, "Kwanini nikupe wewe Sh 20,000 wakati duka la pale linalojulikana linauza Sh 15,000?"
Kama huna jina kubwa linalompa mteja uhakika wa ubora na huduma baada ya mauzo, kuweka bei kubwa ni sawa na kumfukuza mteja mlangoni.
Jinsi ya Kucheza na Mzani wa Bei
Ili biashara yako ipumue na ikue, unapaswa kuzingatia mambo haya matatu:
Tathmini Mzunguko Wako: Kama unajua kwa siku unapata wateja wachache (kwa mfano unatoa huduma za ushauri au unauza fenicha), basi faida yako kwa kila mteja lazima iwe kubwa kulingana na thamani unayotoa.
Jenga Thamani (Value): Badala ya kupandisha bei kwa sababu tu unataka faida, ongeza thamani. Mteja akiona anapata huduma bora, ufungaji (packaging) mzuri, na uaminifu, hatajisikia vibaya kulipa zaidi.
Usishindane kwa Bei Tu: Biashara inayoshindana kwa kushusha bei pekee huwa haina maisha marefu. Shindana kwa kutoa suluhisho ambalo washindani wako hawana.
Hitimisho
Uchumi wa biashara unakutaka uwe na jicho la tatu. Usikimbilie kuuza bei ndogo ikiwa huna uwezo wa kuuza kwa wingi sana, na usiweke bei ya "kifahari" wakati bado hujajenga jina la kuaminika.
Pata usawa kati ya Gharama zako, Thamani unayotoa, na Mahitaji ya soko.
Kumbuka: Lengo la biashara si kupata wateja wengi tu, bali ni kupata faida itakayofanya biashara iendelee kuwepo kesho.
IMEANDIKWA NA
Paul Chengula
0714 260266

Maoni
Chapisha Maoni