MAMBO SABA (7) YA KUZINGATIA KABLA HUJAANZISHA BIASHARA MPYA


Kuanzisha biashara ni uamuzi mkubwa na mzuri ambao huwa unahitaji kujiandaa na kuwa na mpango makini. 

Kuna mambo kadhaa ya kuzingatia kabla hujaanzisha biashara mpya ambayo yanaweza kufanya biashara yako ikafanikiwa au ikafa ambayo ni muhimu kuyafahamu


Katika andiko hili tutangalia mambo kadhaa ya kuzingatia kabla hujafanya maamuzi hayo na ni kwa namna gani yatakusaidia ufikie malengo yako.

1. WAZO LA BIASHARA YAKO

Jambo la kwanza na la muhimu la kuzingatia kabla ya kuanzisha biashara mpya ni wazo la biashara unayotaka kuanzisha. 


Wazo la biashara ndio msingi wa biashara yako kwani unatakiwa uwe na wazo la biashara linaloeleweka vizuri.

Wazo lako la biashara ni muhimu lijibu maswali haya:

  • Bidhaa au huduma utakayotoa ni ipi?
  • Kwa namna gani bidhaa yako itatatua changamoto za watu au kukidhi mahitaji yao?

  • Ni kwa namna gani huduma yako itatofautiana na ya wenzako?

Wazo lako la biashara ni muhimu pia likatokana na ujuzi ulio nao pamoja na jambo ulilo na hamasa nalo kufanya(passion). 

Ni muhimu kufurahia unachokifanya,na ujiamini kwa kile unachowapa au kuwahudumia wateja wako.


2. UZOEFU NA UJUZI WAKO

Jambo lingine la msingi la kuzingatia kabla hujaanzisha biashara ni uzoefu au ujuzi juu ya biashara unayotaka kuanzisha. 

Ni muhimu kuwa na ujuzi,ufahamu na uzoefu wa hiyo biashara unayotaka uanzishe ili ifanikiwe.


Na ni muhimu uwe tayari pia kujifunza mambo mbalimbali yanayohusu biashara unayotaka kuifanya. 

Ujuzi wa muhimu kuwa nao ni kama vile ujuzi wa uongozi,ujuzi wa namna ya kufanya masoko,ujuzi wa namna ya kutatua migogoro ya wateja n.k


Unaweza ukaupata ujuzi wa namna ya kufanya biashara kwa njia mbalimbali kama vile kujifunza kwa wazoefu wanaofanya biashara kama yako,kusoma vitabu mbalimbali,kuhudhuria semina na workshop mbalimbali au kutafuta washauri juu ya biashara husika.


3. SOKO/UHITAJI WA BIASHARA YAKO

Jambo lingine la msingi la kuzingatia kabla hujaanzisha biashara ni soko au uhitaji wa kile unachotaka kuuza.

 

Unatakiwa ufanye utafiti wa kutosha na soko ili uweze kutambua mahitaji na tabia za wateja wako watarajiwa kuhusiana na bidhaa au huduma unayotaka kuuza.


Ni vizuri ukafanya tathimini juu ya uhitaji wa bidhaa au huduma yako na na namna gani inatakiwa kubadilika kutokana na muda na mazingira husika juu ya kile unachouza.


4. GHARAMA ZA UANZISHAJI

Kitu kingine cha msingi cha kuzingatia kabla hujaanzisha biashara mpya ni kuzingatia gharama za kuanzia za kuanzisha biashara yako.

Haya ni matumizi ya lazima ambayo ni muhimu kuyajua kabla hujaanza biashara husika. 

Matumizi haya yanaweza kuwa kama vile vifaa au mashine,vibali na leseni za biashara,gharama za masoko


Vilevile kuna gharama za kuzingatia kama vile pango,mishahara,nakadhalika. 

Ni muhimu ukafahamu gharama hizi ili ujue ni kiasi gani angalau unatakiwa kuwa nacho kabla hujaanza bishara yako.


5. MTAJI WAKO

Jambo lingine la msingi la kuzingatia kabla ya kuanzisha biashara ni kuzingatia mtaji wako. 

Mtaji ni kiasi au chanzo cha fedha ambazo utapaswa kuwa nazo ili uweze kuanzisha biashara yako.


Utatakiwa kuwa na kiasi fulani cha fedha ambacho kitakava gharama zako za uanzishaji wa biashara mpaka pale biashara yako itakapoanza kutengenenza faida.


 Ni muhimu kufahamu pia fedha hizi utazipata wapi ili kuanzisha biashara yako.

Unaweza kupata fedha za kuanzisha biashara yako kutoka vyanzo mbalimbali kama vile akiba yako binafsi ambayo umekua ukitunza,kupata mkopo mahali,au kupata fedha toka kwa muwekezaji fulani.



6. WASHINDANI WAKO

Jambo lingine la msingi ambalo unapaswa kulizingatia ni ushindani wa biashara yako unayotaka kuanzisha. 

Washindani wako ni wale watu au biashara zinazotoa bidhaa au huduma ambayo nawe unataka kuanzisha.


Ni muhimu ukawafahamu washindani wako wa moja kwa moja na wale ambao sio wa moja kwa moja na ukafanya tafiti ili kujua madhaifu yao  na nguvu yao sokoni.


Na wewe pia unatakiwa ujue ni kwa namna gani utajitofautisha nao ili uweze kupenya kwenye soko husika kwa kuja na mikakati mipya ili uweze kuingiza bidhaa au huduma yako kiurahisi.


7. ENEO LA KUFANYIA BIASHARA YAKO

Hili ni jambo la msingi la kuzingatia kabla hujaanzisha biashara yako. 

Unapaswa kujua ni eneo lipi utakua unatumia kufanya biashara yako kama ni eneo la kawaida au online. 

Au biashara yako itapatikana kawaida na online pia.

Ni muhimu kufahamu ni kwa namna gani biashara yako itapatikana kiurahisi na kujulikana kwenye eneo ulilopo,na sheria na taratibu mbalimbali za eneo unapoweka bishara yako. 


Je utawezana na gharama za uendeshaji wa biashara yako kulingana na eneo unaloweka au kuanzisha biashara yako.

Je utamudu gharama za Maisha za eneo au mahali unapotaka kuanziasha biashara yako n.k   

Na je ushindani wa soko upoje na utauweza kwenye hilo eneo unalotaka kuanzisha biashara yako?

Je vibali na leseni za biashara zinapatikana kiurahisi mahali au eneo unalotaka kufanya biashara yako? Hayo ni baadhi ya maswali unatakiwa kujiuliza kabla hujaanzisha biashara husika.


Hayo ni baadhi ya mambo muhimu ya kuzingatia kabla hujaanzisha biashara yako mpya. 

Kumbuka kuanzisha biashara ni jambo la muhimu na lenye hamasa kubwa na watu wengi huwa wanapenda wawe na biashara zao ili kuweza kutimiza malengo yao mbalimbali.


Lakini unapaswa kujua kuwa biashara huwa zina ambatana na hatari ya kutoendelea kutoakana na sababu mbalimbali ambazo zinasababisha biashara zisiendelee.


Kwa kuzingatia mambo hayo saba na mengine mengi ambayo unaweza kuyazingatia itakufanya uwe na uwezekano mkubwa wa biashara yako kufanikiwa kwani utakua umejiandaa vyakutosha kukabiliana na changamoto mbalimbali na ni Imani yetu kuwa andiko hili litakusaidia.



IMEANDIKWA NA

Mchumi Consulting 

(0714 260266 / 0769 218125)

WASILIANA NASI LEO

BONYEZA HAPA KUONA HUDUMA ZETU NYINGINE

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

FAIDA ZA KUWA NA KAMPUNI NA NAMNA YA KUGAWA HISA NA KUISAJILI HAPA TANZANIA