MIKAKATI 6 YA KUFANYA ILI KUONGEZA MAUZO YA BIDHAA AU HUDUMA UNAYOUZA
Mauzo mengi ni miongoni mwa malengo makuu na ya msingi kwa kila biashara. Hapa ina maana pale unapopata mauzo makubwa vilevile,utapata faida kubwa kwenye biashara husika.
Sasa ni namna gani unaweza kufikia malengo ya kuwa na mauzo makubwa kwenye kile unachokiuza katika zama za ushindani mkubwa wa soko? Inatakiwa ujue mikakati na mbinu kadhaa za kukuwezesha kuuza zaidi na hivyo kuongeza faida zaidi.
Katika blog post hii tutaelezea njia na mbinu kadhaa ambazo huwa zinaleta matokeo makubwa hasa pale unapotaka kuongeza mauzo zaidi.
1. UZA BIDHAA/HUDUMA YA NYONGEZA (Cross sell)
Unaweza kutumia mbinu au mkakati huu pale unapotaka kuongeza mauzo zaidi kwa kumuuzia mteja bidhaa ya nyongeza inayoendana na bidhaa au huduma aliyokwisha kununua au aliyo na mpango wa kununua.
Hapa unatakiwa ugundue hitaji la mteja juu ya bidhaa au huduma anayotaka na kumshauri achukue na bidhaa nyingine inayoendana na bidhaa anayotaka. Mfano, Kama unauza laptop unaweza kuuza hapo hapo na betri ya ziada,headphones, au begi la kubebea laptop.
Au unauza smartphone unaweza kumuuzia na kumshawishi mteja anunue na protector. Kama unatoa huduma za kihasibu unaweza kumuuzia mteja na huduma za ushauri wa kodi pia. Hii itafanya uongeze mauzo zaidi na zaidi kwenye kile unachouza.
2. WEKA BEI ZA VIFURUSHI(Price packages)
Kuweka bei katika mfumo wa vifurushi huwa inasaidia kumpa mtu uhuru na ahueni ya kipi achague na anunue. Kama endapo bidhaa au huduma yako unaona ina bei ya juu sana na watu wanaweza shindwa kumudu,basi vunja vunja hizo bei katika mfumo wa malipo ya vifurushi mbalimbali vidogo vidogo.
Hii itasaidia kupata watu wengi watakaonunua bidhaa au huduma yako kuliko kuweka bei moja ambayo ni kubwa na watu wanashindwa kununua.
Mfano wa vifurushi vya bima za afya unakuta kuna vifurushi mbalimbali kuanzia cha bei ya chini na kuendelea na vinapewa majina na madaraja mbalimbali. Mfumo huu sio unaweza kufanya kazi kwenye kila aina ya bidhaa au huduma zote.
3. WAJALI WATEJA ULIO NAO SASA
Ni rahisi sana kuwabakiza na kuwauzia wateja wako uliona nao(wale uliowahi kuwauzia) Kumbuka kuwa ni kazi kubwa kumpata mteja mpya ambae atakuamini kwani huenda hakujui na hajawahi kununua bidhaa au huduma yako.
Hivyo ni muhimu sana kuwajali na kuwathamini wateja ulio nao sasa. Unaweza ukawatumia wateja wako ulio nao sasa ili wakuongezee mauzo zaidi kwa kukusemea vizuri biashara yako kwa marafiki na familia zao.
Hii itakupunguzia gharama za kuuza lakini kwa kuingia gharama kubwa kupata hayo mauzo. Wajali wateja wako kwa kuwapa bidhaa za bure mara moja moja,kuwapa bonas,na vilevile kuwapa mapunguzo ya bei kwenye huduma unazouza au bidhaa.
Jenga mahusiano mazuri na wateja wako na waombe wakupe feedback juu ya huduma au bidhaa uliyowauzia ili kuweza kuboresha zaidi kama endapo kuna dosari.
4. WAPE WAIJARIBU KWANZA(Free trial)
Kama utakua mzoefu kidogo wa huduma zinazotolewa hasa mtandaoni na biashara au makampuni makubwa ni kutoa huduma kwa kipindi fulani cha majaribio kabla mteja hajanunua.
Hii inarahisisha kupata wateja wengi kwani watakua na muda wa kuijaribisha huduma au bidhaa yako kwanza kabla hawajanunua. Tambua kua hofu kubwa ya mteja yoyote ni kukosea kufanya manunuzi ya bidhaa au huduma fulani.
Sasa ukimpa ahueni kuwa hii bidhaa unaweza pata muda wa kuijaribisha baada ya hapo ndio ufanye ununue huwa inavutia wateja wengi sana. Kuwapa wateja free trial sio lazima mteja aondoke na bidhaa,unaweza kumpa sample kidogo akajaribu.
Kwa lugha nyepesi ya Kiswahili tunasema “waonjeshe” kwanza. Hujawahi ona mtu anauza sabuni ya maji lakini kabla hajakuuzia anakuachia sample kidogo ili ukajaribu ufanisi wake kwanza kabla ya kununua?
Hujawahi ona muuza karanga anakuonjesha kwanza kabla ya kukuuzia? Hii ni mifano ambayo inaweza kutoa picha nyepesi ya maana ya “free trial” kwenye kitu unachouza. Tumia mkakati huu kama endapo utaona inafaa kwenye bidhaa au huduma unayotoa,ili mteja ajenge kukuamini kwanza baada ya hapo atanunua zaidi na zaidi
5. ITANGAZE ZAIDI BIDHAA/HUDUMA YAKO
Huenda moja ya sababu inayofanya uendelee kuwa na mauzo madogo ya bidhaa au huduma unayouza ni idadi ndogo ya wateja ulionao. Huenda soko lako bado ni la watu wale wale waliokuzoea.
Sasa weka mipango na mikakati mipya ya namna ya kuwafikia wateja wengine wapya kabisa ambao watanunua bidhaa au huduma yako. Njia za kujitangaza zipo nyingi sana itategemeana na mazingira uliyopo,aina ya bidhaa au huduma na nyingine nyingi.
Unaweza changanya mbinu za kujitangaza kama vile kutumia wateja wako walewale wakusaidie kuleta wateja wengine,na vilevile anza kutengenenza uwepo wako kwa kutumia njia ya mitandao ya kijamii ambako huko kuna watu wengi wa aina mbalimbali ambao wanaweza kupenda bidhaa au huduma yako.
6. UZA JINA(BRAND) KWANZA KABLA YA KUUZA BIDHAA AU HUDUMA
Moja ya jambo la msingi ambalo litakusaidia kuuza bidhaa au huduma yako kiurahisi na kuongeza mauzo ni kujikita kwanza katika kuuza brand(jina) yako kwanza kabla ya bidhaa au huduma.
Ni vizuri ukajiweka katika mazingira ambayo watu wataelewa ni nini unafanya,na bidhaa yako ina utofauti gani katika kutoa suluhisho ukilinganisha na washindani wako. Jikite katika kujitofautisha ili kuleta uthamani wa brand yako ili watu waone kuna umuhimu wa kuambatana na brand yako.
Usiishie kuwa muuzaji tu bali weka mazingira ya kuwa mtaalamu wa kuwaelekeza au kutoa ushauri kwa watu wa namna unavyoweza kutoa suluhisho kupitia bidhaa au huduma yako. Watu wafahamu eneo lako la ubobevu ni wapi ili waweze kujua kuwa wewe ni mtu sahihi wa kuwapa huduma au bidhaa wanayoihitaji.
Jitofautishe na wauzaji wengine katika namna wanauza na jinsi wana hudumia wateja n.k Usikimbilie tu kuwinda kupata fedha kwa kutangaza tu bidhaa au huduma zako kabla hujalitangaza jina(brand) lako.
Tengenenza utambulisho wako wa kipekee sokoni kwa kutumia njia mbalimbali kama vile kuwa na logo inayokutambulisha,social media accounts,websites na kuwapa watu elimu fulani bure inayohusiana na bidhaa au huduma yako. Hii itasaidia kuongeza mauzo ya bidhaa au huduma unayotoa.
HIYO ni baadhi ya mikakati unayoweza kuifanya ili kuongeza mauzo ya kile unachouza. Na kumbuka kuna njia nyingine unaweza kuzitumia kuongeza mauzo kulingana na aina ya bidhaa au huduma na eneo ulilopo pamoja na kutumia ujuzi na uzoefu mwingine.
IMEANDIKWA NA
Mchumi Consulting
0714260266
MFANYABIASHARA JIUNGE BURE NA GROUP LETU LA WASAP ILI KUPATA HUDUMA NA MASOMO YETU MUDA WOTE👇👇
BONYEZA HAPA KUJIUNGA NA GROUP LETU LA WASAP BURE
.jpeg)
Maoni
Chapisha Maoni