JUA FAIDA ZA KUFANYA UWEKEZAJI KWENYE HISA ZA MAKAMPUNI
Pointi ya msingi ya Warren Buffett ilikua ni msisitizo juu ya umuhimu wa kufanya uwekezaji ambao unaweza kukuingizia mapato hata bila uwepo wako(passive income).
Yaani umefanya uwekezaji watu wengine au system zinaendelea kukuingizia kipato bila hata wewe kuwepo eneo husika.
Fikiria umefanya uwekezaji halafu mwisho wa mwezi au mwisho wa mwaka pesa inaingia tu kwenye akaunti yako bila wewe kutumia nguvu kubwa na muda.
Katika andiko hili tutaelezea aina mojawapo ya uwekezaji ambao unaweza kukuingizia mapato bila uwepo wako ingawa inahitaji nguvu na jitihada kubwa mwanzoni wakati wa kuwekeza.
Tutaangalia nini maana,faida,na ugumu wa kuwekeza kwenye Hisa za makampuni. Na vilevile tutaona ni mambo gani ya msingi ya kuzingatia kabla hujawekeza katika Hisa.
NINI MAANA YA HISA
Hisa ni sehemu ya umiliki wa kampuni.
Mwekezaji anayenunua hisa za kampuni,ananunua haki ya umiliki wa kampuni hiyo. Kwahiyo kama kampuni ina hisa milioni moja na mwekezaji anamiliki 10,000 basi mwekezaji huyo anamiliki asilimia moja (1%) ya kampuni husika.
Haki za mwanahisa ni pamoja na kushiriki katika kutoa maamuzi ya kampuni katika mikutano mikuu ya wanahisa.
Na pia mwanahisa ana haki ya kupata gawio na faida ya kampuni na vilevile anaweza kuuza hisa zake kwa faida pale ambapo kuna ongezeko la thamani ya hisa.
BEI YA HISA
Bei ya hisa za kampuni ambazo zimeorodheshwa katika soko la Hisa hubadilika kwa wakati kulingana na nguvu ya soko ambapo thamani ya hisa huweza kuongezeka au kupungua.
Aidha bei ya hisa inategemea utendaji wa kampuni husika na hali ya uchumi kwa ujumla. Hivyo ni muhimu mnunuzi wa hisa kujiridhisha na mwenendo wa utendaji wa kampuni kabla ya kuwekeza kwenye hisa zake.
Na mauzo ya awali ya hisa za kampuni kwa umma hufanyika kupitia soko la awali (primary market).
Na baadae hisa za kampuni huorodheshwa katika soko la hisa(secondary market) ambapo wawekezaji hushiriki kupitia watendaji wa masoko ya mitaji wenye leseni za mamlaka ya masoko ya mitaji na dhamana(CMSA)
FAIDA ZA UWEKEZAJI KWENYE HISA
- Kupata gawio kutokana na faida ya kampuni
- Ni njia ya kuweka akiba-(kununua hisa ni kuwekeza kwa matumizi ya baadae)
- Kumpatia mwekezaji fursa ya kutoa maoni yake kwenye mkutano mkuu wa kampuni.
- Hisa pia zinaweza kutumika kama dhamana(collateral) ya kupata mkopo toka taasisi ya fedha.
UGUMU KATIKA UWEKEZAJI KWENYE HISA
- Mabadiliko ya soko (kupanda na kushuka) kunaweza kuathiri moja kwa moja thamani ya hisa za kampuni husika,hivyo kupata hasara
- Utendaji wa kampuni ni kigezo mojawapo cha kupata faida au hasara kwenye uwekezaji kwenye hisa. Hii ina maana kwamba kama endapo Kampuni imetengeneza hasara jua nawe muwekezaji unakua ndani ya hasara hiyo. Unakua huna uhakika wa moja kwa moja wa kupata gawio lako.
- Pia Hisa huwa zinaambatana na kodi ya serikali pale unapopewa sehemu ya faida yako na hivyo kupunguza mapato yako toka kwenye uwekezaji uliofanya.
KIPI CHA KUZINGATIA KABLA YA KUWEKEZA KWENYE HISA
Kabla hujafanya maamuzi ya kuwekeza katika Hisa ni vizuri ukafahamu baadhi ya mambo muhimu ili usije ukapata hasara.
Kwani ni mara nyingi watu wakisikia kuna kuwekeza kwenye Hisa wanaamini watapata faida muda wote,hivyo ni muhimu kuzingatia mambo yafuatayo:
- Fanya utafiti wa Kampuni unayotaka ununue Hisa zake. Hakikisaha unajua kiundani zaidi mambo mbalimbali kuhusu kampuni husika. Kama huwezi kujua namna ya kufanya utafiti wa Kampuni hiyo basi pata usaidizi toka kwa wataalamu wa masuala ya uwekezaji
- Chagua kuwekeza kiasi ambacho kitaendana na ustahimilivu wako wa hatari kama ikitokea(kiasi ambacho upo tayari kupoteza kama endapo itatokea hasara)
- Tawanya uwekezaji wako(diversity your share portifolio). Hapa tunamaanisha usifanye uwekezaji wako kwenye kampuni moja pekee kwa kuweka fedha zako zote.
Hii itakuletea shida sana kama endapo Kampuni husika itapata hasara na fedha zote uliweka kwenye kampuni hiyo.
- Fuatilia kwa ukaribu hali ya soko ili uweze kufanya maamuzi ya kuwekeza kutokana na hali ya soko lilivyo katika kipindihali ya soko lilivyo katika kipindi husika


Maoni
Chapisha Maoni