Je, Hisa Unazotaka Kununua Zina 'Mfereji wa Kinga'? Usiwekeze Bila Kusoma Hii!
Hebu rudi nyuma kidogo hadi karne ya 15. Fikiria jumba kubwa la kifalme (Castle) lililojaa dhahabu na vito vya thamani.
Ili kuzuia maadui wasiingie ndani na kuiba mali hizo, wafalme walichimba mfereji mpana sana wa maji (MOAT) kuzunguka lile jumba, kisha wakaweka mamba ndani ya maji hayo. Adui yeyote akijaribu kuvuka, anashindwa na kuliwa!
Kwenye ulimwengu wa hisa, wewe ni mfalme, na pesa yako ndiyo dhahabu iliyo ndani ya kampuni. Kampuni yoyote unayowekeza lazima iwe na "Moat" ya kiuchumi.
Kama kampuni haina mfereji huu wa kuilinda, washindani wataingia, wataiba wateja wake, na mwisho wa siku kampuni itakufa—na wewe utapoteza mtaji wako.
Je, unajuaje kama kampuni ina mfereji imara (Wide Moat) au ina shimo dogo tu ambalo adui anaweza kuruka?
Hapa kuna aina 5 za MOAT unazopaswa kuzitafuta kwa makini kabla ya kuwekeza:
1. Nguvu ya Jina (The Brand Moat)
Hii ni aina ya ulinzi ambapo jina la kampuni limejijenga kiasi kwamba mteja yuko radhi kulipa bei kubwa zaidi kwa sababu tu ya imani aliyonayo.
Jina imara linampa mwekezaji amani kwa sababu kampuni ina uwezo wa kupandisha bei (Pricing Power) bila kupoteza wateja.
Kwa mfano, duniani kote tunaiona kampuni kama Apple. Watu wako radhi kupanga mstari usiku kucha kununua simu ya mamilioni ya shilingi, wakati kuna simu nyingine za bei nafuu zinazofanya kazi zilezile. Hapa nyumbani Tanzania, tunaweza kuona nguvu hii kupitia Azam.
Kwa mtanzania wa kawaida, jina la Azam ni alama ya uhakika kuanzia kwenye vinywaji hadi vyakula. Hata washindani wapya waje kwa kasi gani, kumuondoa mteja kwenye himaya ya Azam ni mtihani mzito sana.
2. Gharama za Kubadili (Switching Costs Moat)
Mfereji huu hautengenezwi na bidhaa pekee, bali na "usumbufu" wa kuhama. Inatokea pale ambapo inakuwa ni kero, gharama, au hatari kwa mteja kuacha kutumia huduma ya kampuni moja na kwenda kwa nyingine.
Ikiwa mteja anahisi itachukua muda mrefu au itakuwa usumbufu mkubwa kuhama, kampuni hiyo inakuwa na ulinzi wa chuma.
Fikiria makampuni kama Microsoft. Ofisi nyingi hutumia mifumo yao; wakiamua kuhama leo, itabidi wafundishe wafanyakazi upya mifumo mingine, jambo ambalo ni gharama na usumbufu mkubwa.
Hali kadhalika kwenye sekta ya kibenki nchini, mfano NMB au CRDB. Ikiwa mteja ana akaunti ya mshahara, makato ya bima, na mikopo kwenye benki fulani, uwezekano wa yeye kuhama ni mdogo sana. Ule usumbufu wa kuanza upya mahali pengine ndio unaolinda faida ya benki hizo.
3. Athari za Mtandao (The Network Effect Moat)
Huu ni mmoja kati ya mifereji imara zaidi duniani. Thamani ya huduma huongezeka kadiri watu wengi zaidi wanavyoitumia. Katika mfumo huu, mteja mpya anapojiunga, anawafanya wateja wa zamani wawe na thamani zaidi.
Chukulia mfano wa Visa au Mastercard. Maduka yote yanapokea kadi hizi kwa sababu watu wote wanazo, na watu wote wanazo kwa sababu maduka yote wanazipokea. Hapa nchini, mfano bora ni M-Pesa.
Kwa nini watu wengi wanaitumia? Ni kwa sababu wakala yupo kila kona na kila mtu unayetaka kumtumia pesa tayari yumo kwenye mtandao huo.
Hata kampuni nyingine ikitoa huduma bila makato, ni vigumu kuivunja hii "Network Effect" kwa sababu kila mtu tayari yuko Vodacom.
4. Gharama Nafuu za Uzalishaji (Cost Advantage Moat)
Kama kampuni inaweza kuzalisha bidhaa kwa gharama ya chini sana kuliko mshindani wake, inapata uwezo wa kutawala soko.
Hii hutokana na kampuni kumiliki malighafi zake, kuwa na teknolojia ya kisasa, au kuwa na mikataba ya kipekee inayopunguza matumizi.
Duniani, Amazon imetawala kwa sababu ya kuwa na maghala makubwa na mfumo wa kidijitali unaopunguza gharama za uendeshaji.
Katika mazingira yetu, makampuni kama Twiga Cement au Dangote Cement yana faida hii. Kwa kumiliki viwanda vikubwa na machimbo ya chokaa karibu na maeneo ya uzalishaji, yana uwezo wa kuzalisha simenti kwa gharama ndogo ambayo mshindani mdogo anayesafirisha malighafi kutoka mbali hawezi kuifikia.
5. Siri za Biashara na Leseni (Intangible Assets Moat)
Aina hii ya Moat ni kama "pingu" za kisheria kwa washindani. Hapa kampuni inamiliki kitu ambacho kisheria mshindani haruhusiwi kukiiga, kama vile Haki Miliki (Patents) au Leseni za Serikali.
Makampuni makubwa ya dawa duniani hutumia mabilioni ya dola kugundua dawa, kisha hupata ulinzi wa kisheria wa miaka mingi ambapo hakuna mwingine anaruhusiwa kutengeneza dawa hiyo.
Hapa Tanzania, tunaona hili kwenye sekta ya madini kupitia makampuni kama Barrick (Twiga Minerals).
Wanapopewa leseni ya kipekee ya kuchimba kwenye eneo fulani, hakuna mshindani mwingine anayeweza kuingia. Leseni hiyo ya serikali inakuwa mfereji wao wa kulinda dhahabu na faida yao.
Mwisho
Unapotafuta hisa ya kununua kwenye soko la hisa la Dar es Salaam (DSE), usijiulize tu "Je, hii kampuni inapata faida?" Badala yake, chunguza kwa kina: "Je, hii kampuni ina MOAT gani ya kuizuia isiliwe na washindani?"
Kumbuka, kampuni yenye mfereji mpana na mamba wakali ndiyo itakayokuhakikishia utajiri wa kudumu na usalama wa uwekezaji wako.
Imeandikwa na
Paul Chengula
0714 260266
PATA KITABU KUHUSU MUONGOZO WA UWEKEZAJI KWENYE HISA HAPA

Maoni
Chapisha Maoni