MAKOSA 5 YANAYOFANYA BIASHARA IONGEZE MAUZO LAKINI IPOTEZE PESA

 

Kuna tofauti kubwa kati ya biashara inayouza sana na biashara inayotengeneza pesa.

Wakati mwingine unaweza kuona bidhaa zinatoka dukani kila siku, oda zinaongezeka, wateja wanaongezeka, na fedha nyingi zinaingia. Ukiangalia kwa haraka unaweza kusema:

“Biashara hii inafanya vizuri sana!”

Lakini si kila fedha inayoingia kwenye biashara ni faida.

Unaweza kuongeza mauzo kutoka TZS 30 milioni hadi TZS 50 milioni, lakini mwisho wa mwezi ukawa na pesa kidogo kuliko ulivyokuwa na TZS 30 milioni.

Kwa nini?

Kwa sababu biashara haipotezi pesa kwa kukosa mauzo tu. Wakati mwingine inapoteza pesa kwa namna inavyofanya hayo mauzo.

Haya ndiyo makosa 5 ambayo mfanyabiashara anapaswa kuyaangalia.


1. KUKIMBIZA MAUZO BILA KUANGALIA FAIDA (PROFIT)

Mfanyabiashara anaweza kuweka lengo:

“Mwezi huu lazima tufikishe TZS 100 milioni za mauzo.”

Hilo ni jambo zuri. Lakini siyo mwisho wa hadithi.

Jiulize pia:

“Hizo TZS 100 milioni zimetuachia faida kiasi gani?”

Mfano, biashara inaweza kuuza bidhaa za TZS 100M, lakini gharama ya kununua bidhaa hizo ikawa TZS 85M.

Hapo umebaki na TZS 15M kabla hata ya kuangalia gharama nyingine za biashara.

Kama una kodi, mishahara, usafiri, matangazo, kamisheni na gharama nyingine, hiyo TZS 15M inaweza kupungua zaidi.

Kwa hiyo:

Usifuatilie mauzo pekee. Fuatilia mauzo yenye faida (Profitable Sales).


2. KUTOA PUNGUZO (DISCOUNT) ILI KUFIKISHA LENGO LA MAUZO

Kutoa punguzo (Discount) inaweza kusaidia kuongeza mauzo, lakini punguzo lisipotumika vizuri linaweza kula faida yako.

Mfano:

Ulikuwa unauza bidhaa kwa TZS 100,000.

Ukaamua kutoa punguzo na kuuza kwa TZS 85,000 ili kuvutia wateja wengi.

Mauzo yakaongezeka.

Unaweza kufurahia kusema:

“Punguzo letu limefanya kazi!”

Lakini swali ni:

“Baada ya punguzo hilo, faida inayobaki iko kiasi gani?”

Kama umeongeza mauzo lakini kila mauzo yanakuachia faida ndogo sana, huenda umeongeza Revenue bila kuongeza Profit.

Si kila mauzo ni mauzo mazuri (Not every sale is a good sale).

Wakati mwingine ni bora kuuza kidogo kwa faida nzuri kuliko kuuza sana kwa faida ndogo sana.


3. KUPUUZA GHARAMA YA KUMPATA MTEJA

Mteja mpya haingii kwenye biashara bila gharama.

Unaweza kutumia fedha kwenye:

  • Matangazo

  • Punguzo

  • Kamisheni ya mauzo

  • Usafiri

  • Simu

  • Mikutano

  • Mitandao ya kijamii

  • Muda wa timu ya mauzo

Hizi zote zinaweza kuwa sehemu ya Gharama ya Kumpata Mteja (Cost of Acquisition).

Mfano:

Umempata Mteja anayekuletea TZS 5M.

Unaweza kusema:

“Mteja huyu ni mzuri.”

Lakini kama umetumia TZS 2M kumpata na kumshawishi afanye manunuzi, unahitaji kuangalia picha nzima.

Mteja anayekuletea mapato makubwa siyo lazima akuletee faida kubwa.

Ndiyo maana biashara inapaswa kujua:

“Tumetumia kiasi gani kumpata Mteja huyu, na baada ya gharama hizo ametubakishia kiasi gani?”


4. KUFIKIRI MTEJA MKUBWA NI MTEJA BORA

Hili ni kosa lingine.

Mteja anayekununulia TZS 100M kwa mwaka anaweza kuonekana kuwa Mteja bora kuliko anayekununulia TZS 40M.

Lakini si lazima iwe hivyo.

Mteja wa TZS 100M anaweza:

  • Kuomba punguzo kubwa

  • Kuhitaji huduma nyingi

  • Kuwa na gharama kubwa za kupeleka bidhaa

  • Kuwa na malalamiko mengi

  • Kuhitaji ufuatiliaji mwingi

Wakati Mteja wa TZS 40M anaweza kuwa rahisi kumhudumia na akawa na faida nzuri zaidi.

Kwa hiyo usiangalie tu:

“Mteja huyu anatuletea mapato kiasi gani?”

Angalia pia:

“Mteja huyu anatuletea faida kiasi gani?”

Hii ndiyo tunaita Faida ya Mteja (Customer Profitability).

Mteja mkubwa si lazima awe Mteja mwenye faida zaidi.


5. KUPIMA TIMU YA MAUZO KWA MAUZO PEKEE

Mfanyakazi wa mauzo anaweza kufikisha lengo lake la TZS 50M na kuonekana amefanya vizuri.

Lakini jiulize:

Alitoa punguzo kiasi gani?

Faida iliyopatikana ilikuwa nzuri?

Gharama ya kumpata Mteja ilikuwa kiasi gani?

Mteja aliyeletwa ana faida nzuri?

Kama timu ya mauzo inafundishwa tu:

“Ongeza mauzo!”

inaweza kuanza kutafuta wingi wa mauzo bila kuangalia ubora wa mauzo.

Badala yake, timu ya mauzo inapaswa kuelewa:

“Tunataka kuongeza mauzo, lakini mauzo yenye faida nzuri na wateja wenye faida.”

Hapo ndipo mauzo yanaanza kuwa ukuaji wa biashara (Business Growth), siyo kuongeza namba tu.


KWA HIYO, MFANYABIASHARA AANGALIE NINI?

Usiishie kwenye Mapato (Revenue) pekee.

Angalia pia:

Faida Ghafi (Gross Profit) – Baada ya kutoa gharama za moja kwa moja za bidhaa au huduma, tumebaki na kiasi gani?

Faida ya Mchango (Contribution Margin) – Mauzo haya yanachangia kiasi gani kwenye gharama nyingine za biashara na faida?

Gharama ya Kumpata Mteja (Cost of Acquisition) – Tumetumia kiasi gani kumpata Mteja?

Faida ya Mteja (Customer Profitability) – Baada ya gharama zote zinazohusiana na Mteja, anatuletea faida kiasi gani?

Hizi namba zinakusaidia kuona ukweli ambao Mapato (Revenue) pekee hayawezi kukuonyesha.


MWISHO WA SIKU...

Kuuza zaidi ni jambo zuri.

Lakini kuuza zaidi bila kuangalia faida kunaweza kuwa mtego.

Usijiulize tu:

“Tumeuza kiasi gani?”

Jiulize pia:

“Tumepata faida kiasi gani?”

“Faida kwenye kila mauzo iko vipi?”

“Tumetumia kiasi gani kumpata Mteja?”

“Ni wateja gani wanaotuletea faida zaidi?”

Kwa sababu:

Mapato (Revenue) yanaweza kukufanya uonekane unafanya vizuri. Lakini faida (Profit) ndiyo inakuonyesha kama biashara inafanya vizuri kweli.

Mauzo mengi siyo faida kubwa (Big sales aren't the same as big profit).

👉 Lengo si kuuza zaidi tu. Lengo ni kuuza zaidi kwa namna inayofanya biashara ibaki na faida.


IMEANDALIWA NA

Paul Mchumi

0714 260266


Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

JINSI YA KUWEKEZA NA KUMILIKI HISA ZA MAKAMPUNI YA TANZANIA

KITABU CHA MISINGI YA UWEKEZAJI:FAHAMU SIRI ZA KUANZA KUWEKEZA KWENYE HISA NA BOND NA JINSI YA KUEPUKA HASARA

MFAHAMU PAUL CHENGULA