MTEGO WA MUONEKANO Kwanini Ofisi Nzuri Haidhamini Uhai wa Biashara
Kuna huu mtindo wa kisasa umeingia mjini: Mtu anapata mtaji wake wa kwanza, labda ni mafao, mkopo, au kile alichokuwa anasave kwa miaka.
Kitu cha kwanza anachofikiria ni kupata fremu ya kioo, kuweka "gypsum" ya gharama, kununua taa za urembo (spotlights), na kiti cha bosi ambacho kinarudi nyuma.
Kwa nje, biashara inaonekana imeshafanikiwa kabla hata haijaanza. Lakini ukweli mchungu ni huu:
Wateja hawanunui rangi ya kuta, wananunua bidhaa au huduma. Na mbaya zaidi, zile pesa zilizopotea kwenye urembo ndizo zilipaswa kuwa "damu" ya biashara yako.
Hapa ndipo tunapokutana na dhana muhimu ya Cashflow.
Cashflow: Pumzi ya Biashara Yako
Watu wengi wanachanganya kati ya Mtaji na Cashflow.
Mtaji ni kile ulichoanza nacho, lakini Cashflow ni ule uwezo wa pesa kuingia na kutoka kila siku ili mambo yaendelee.
Biashara inaweza kuwa na muonekano wa bilionea, lakini ikakosa Cashflow ya kulipa hata bili ya maji au luku. Hiyo ni biashara inayoelekea shimoni.
Tazama mfano huu:
Tuchukue mfano wa wafanyabiashara wawili wa nguo:
Mjasiriamali A (Mwenye Akili ya Cashflow):
Alianza na chumba kidogo. Alitumia mbao za kawaida tu kutengeneza rafu. Pesa yake kubwa (Milioni 10) aliweka kwenye mzigo.
Kila wiki analeta mzigo mpya kwa sababu ana pesa mkononi. Pesa inazunguka—inaingia na kutoka. Akipata "mwezi mbaya," ana akiba ya kutosha kuendelea.
Mjasiriamali B (Mtego wa Muonekano): Alichukua Milioni 10 ileile. Akatumia Milioni 7 kurekebisha ofisi iwe kama ya Ulaya. Akabakiwa na Milioni 3 tu ya mzigo. Duka ni zuri, lakini rafu zipo nusu tupu.
Nini kinatokea "Mwezi Mbaya" ukifika?
Kwenye biashara, kuna miezi ambayo wateja wanakuwa "wamefunga mikono"—labda ni msimu wa kodi za shule au hali ya uchumi imeyumba.
Hapa ndipo Cashflow inapotofautisha kati ya anayesurvive na anayekufa:
Mjasiriamali B (Mwenye Ofisi Nzuri): Hana pesa mkononi. Kodi ya pango inadaiwa (na duka lake la kioo pango lake ni kubwa).
Hana pesa ya kuweka "Ads" (matangazo) ili kuvuta wateja. Anaanza kupagawa. Anakosa utulivu na anaanza kuuza bidhaa kwa bei ya kutupa ili tu apate pesa ya kula. Anasuffocate (Anakabwa).
Mjasiriamali A (Mwenye Cashflow): Hana presha. Anajua ana mzigo wa kutosha na bado ana "Cash" ya dharura benki.
Haingii gharama kubwa za uendeshaji (Overheads). Hata kama mauzo yatasuasua kwa wiki mbili, biashara yake bado "inapumua."
Pesa Yako Isizikwe Kwenye Maboksi
Kuna mtu aliwahi sema "All their money is sitting in boxes on a shelf." Hili ni kosa kubwa la wafanyabiashara wa Bongo.
Kununua mzigo mwingi sana (Bulk Inventory) ili tu uonekane una duka kubwa ni hatari kama huna uhakika wa soko.
Pesa ikikaa kwenye box stoo, hiyo sio pesa tena—ni karatasi na vitambaa.
Inakuwa pesa pale tu inapouzika. Lakini wakati unasubiri iuzike, mwenye nyumba anataka kodi, na wafanyakazi wanataka mishahara. Kama huna Cashflow, utalazimika kufunga lile duka lako zuri la vioo.
Somo la Leo
Usiogope kuanza mdogo. Usiogope kuanza na ofisi ya kawaida. Uzuri wa ofisi hauwezi kukulipia deni la benki wala mshahara wa mfanyakazi.
Kumbuka:
👉🏻 Cashflow ndio mfalme.
👉🏻Zungusha pesa yako (Keep the money moving).
Usifungie mtaji wote kwenye "stock" au urembo wa ofisi.
Biashara ni mzunguko.
Biashara isiyozungusha pesa, haistahili kuitwa biashara—hilo ni jumba la makumbusho!
IMEANDIKWA NA
Paul Chengula (Paul Mchumi)
0714 260266

Maoni
Chapisha Maoni